Dk. Biteko apongeza mikakati ya kuinua elimu Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko amepongeza Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) pamoja na uongozo wa Jiji la Dodoma kwa mikakati ya kuboresha na kukuza elimu iliyosheheni ubunifu.  Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Dk. Biteko ametoa pongezi hizo leo  Jumamosi wakati akifungua mkutano wa wakuu wa Shule za msingi na sekondari na waratibu elimu Kata ulioandaliwa na Mavunde kwa lengo la kujadiliana changamoto za mhula uliopita na kujipanga na mhula ujao kuanzia mwezi Julai 2024.

Aidha Dk. Biteko ametumia fursa hiyo kuwapongeza walimu wote nchini kwa kazi nzuri wanayofanya katika kujenga kizazi bora kijacho chenye nidhamu,maadili na kujitambua.

“Kama tunataka kujenga taifa lenye ustaarabu, kustahimiliana na lenye amani, mahali pekee pa kuwekeza ni kwenye elimu, mataifa yote yaliyoendelea uwekezaji wake mkubwa upo kwenye elimu,” amesema Dk. Biteko.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda amepongeza hatua hizo za kuwaongezea morali wa kufanya kazi walimu kwa kukutana pamoja na viongozi kujadiliana changamoto za kwenye sekta ya elimu na kuongeza kuwa Serikali inajenga vyuo 64 vya VETA nchi nzima, kampasi za vyuo vikuu kwenye mikoa karibu yote nchini ili kuboresha upatikanaji wa elimu kwenye maeneo jirani.

Akitoa maelezo ya awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Samia Hassan kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya elimu Mkoani Dodoma na kupelekea ongezeko kubwa la ufaulu mkoani Dodoma kwa miaka ya hivi karibuni.

Akizungumza madhumuni ya mkutano huo, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amesema lengo la kukutana na walimu hao ni kujadiliana mafanikio na changamoto za mhula  uliopita na kujipanga na mhula ujao ili tuweze kulitendea.

haki jiji letu la Dodoma kwenye sekta ya elimu kwa kuweka mikakati kabambe ya kuboresha sekta.

Katika mkutano huo Mavunde amekabidhi photocopiers 10 kubwa kwa lengo la kuchapisha mitihani na kuwapunguzia mzigo wazazi wa watoto wa Dodoma Jiji kuchangia fedha za mitihani ya majaribio ya kila wiki.

Related Posts