Iringa. Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce), Dk Fikira Kimbokota amesema Ukimwi bado upo na kuwakumbusha wasomi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya.
Amesema Muce imekuwa ikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo ili kudhibiti maambukizi mapya.
Akizungumza na Mwananchi baada ya mafunzo kwa wahadhiri, wanafunzi na jamii ya chuo hicho, Dk Kimbokota amesema Ukimwi bado upo na jitihada za kuendelea kupambana na ugonjwa huo hazipaswi kupoa.
Amesema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaotekelezwa chini ya Benki ya Dunia (WB) wameanza kutoa elimu ili kujikinga na maambukizi mapya.
“Ukimwi upo tusijisahau, tuendelee kupambana na maambukizi mapya kwani yanaongezeka na yanaleta athari kubwa kwetu,” amesema Kimbokota.
Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai amesema upo uhusiano baina ya Ukimwi na ukatili wa kijinsia.
“Tumekuwa tukitoa elimu ya kujilinda na kujitambua kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kwa sababu wakijisahau wanaweza kutoka vyuoni na Ukimwi na sio elimu waliyoifuata,” amesema Swai.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Muce, Shaban Likondangoma amesema ukatili wa kijinsia, maambukizi ya Ukimwi na afya ya uzazi vinaweza kuwa kikwazo kwenye elimu.
Amesema baada ya tathimini kuonyesha kuwa maeneo hayo ni changamoto, waliona ni muhimu kuandaa mafunzo kwa ajili ya jamii hiyo.
Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Mkoa wa Iringa, Elizabeth Swai amesema wamekuwa wakipokea matukio ya ukatili wa kijinsia toka kwenye taasisi za elimu ya juu jambo linalowalazimisha kutoa mafunzo.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi ya Muce, Sara Mwaipopo amesema ni kweli kwamba wanafunzi wasipofikiwa na elimu sahihi kuhusu masuala hayo wanaweza kuwa changamoto kwao kutimiza malengo yao.