WASHAMBULIAJI Kibu Denis wa Simba na Simon Msuva wa Al Najma wanatarajiwa kuungana timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa uwanjani kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Indonesia na kutoka suluhu, ili kuwahi pambano la kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Zambia.
Wawili hao ni miongoni mwa mastaa 34 walioitwa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ ili kujiandaa na mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia, lakini hawapo kambini hadi sasa huku sababu zikitajwa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Cliford Ndimbo aliliambia Mwanaspoti kuwa, mastaa hao kila mmoja ana sababu ya kutokuwepo kikosini hapo lakini wote wanatarajia kujiunga na Stars kesho Jumanne itakaporejea nchini ili kwenda Zambia kuumana na wenyeji katika mechi ya Kundi E.
“Wachezaji ambao hawaonekani lakini wameitwa, wapo kwenye majukumu mengine lakini watajiunga na timu itakaporejea nchini kutoka Indonesia kisha kwenda Zambia katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia,” alisema Ndimbo.
Kabla ya kauli hiyo ya Ndimbo, Mwanaspoti lilimtafuta moja ya wachezaji wa Stars ambao hawako na timu (jina tunalo) na kueleza sababu za kutokuwa kambini hadi sasa.
“Haya mambo yanachanganya, ujue sikujulishwa mapema. Baada ya kikosi kutangazwa ndio nilijua nimeitwa timu ya taifa ila kabla ya hapo nilikuwa na ratiba zangu nyingine hivyo hilo limenikwamisha,” alisema nyota huyo aliyekiri tayari tatizo hilo limemalizika na atajiunga na timu itakaporejea nchini.
Wachezaji wengine walioitwa Stars, lakini hawapo kambini ni Novatus Dismas, Haji Mnoga na Kelvin John sambamba wengine kutoka Azam na Yanga waliokuwa wakisubiri fainali ya FA kisha watajiunga na timu.
Tanzania na Zambia zilizo kundi E zitacheza mechi hiyo Juni 11, mwaka huu nchini Zambia.