Kouablan afunika Zambia akiwa Simba

Mshambuliaji wa Simba, Fred Kouablan ameibuka mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zambia lakini akiwa nje ya Ligi hiyo kwa muda mrefu.

Kouablan, ameibuka kinara wa mabao Zambia kwa mabao yake 14 ambayo hakuna mchezaji aliyeifikia licha ya straika huyo kuondoka nchini humo tangu Januari kwa ajili ya kujiunga na Simba. Na baada ya kutua Simba, Freddy amefunga mabao sita na hivyo kuwa ameweka kambani mabao 20 ya ligi msimu huu akicheza ligi mbili tofauti.

Ligi ya Zambia ambayo imemalizika jana, Red Arrows imeibuka Mabingwa wa Ligi nchini humo, huku Kouablan aliyekuwa akiitumikia Green Eagles akibeba kiatu cha ufungaji bora.

Arrows imekuwa bingwa Zambia ikimaliza na pointi 72, nafasi ya pili ikishikiliwa na Zesco yenye pointi 59 wakati Power Dynamos ikimaliza na alama 51.

Nyuma ya Kouablan walikuwa Enock Sakala wa Zesco aliyefunga mabao 12, Andrew Phiri wa Muza FC akimaliza na mabao 11 huku washambuliaji wawili wa mabingwa wapya wa nchi hiyo Rick Banda na Sadam Phiri wote wakimaliza na mabao 10 kila mmoja.

Rekodi bora ambayo Kouablan, raia wa Ivory Coast, ameiweka kwenye ligi hiyo ni kuchukua tuzo ya ufungaji bora akitumia mechi 16 pekee kabla ya kutimkia Simba kupitia usajili wa dirisha dogo.

Related Posts