Madeni yatajwa kuchangia changamoto za afya ya akili

Dodoma. Ili kulinda afya ya akili watu wametakiwa kuishi kwenye kiwango cha maisha wanayoyamudu  na kuachana na maisha ya gharama kubwa, ambayo yanawaingiza kwenye madeni wasiyoweza kuyalipa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 02, 2024 na daktari bingwa wa magonjwa na afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Godwin Mwisomba wakati akizungumza na Mwananchi Digital jinsi ya kulinda afya ya akili.

Dk Mwisomba amesema kuishi maisha ya yasiyolingana na kipato cha muhusika yanasababisha kuingia kwenye madeni, ambayo mwisho wake hawezi kuyalipa na kumsababishia sonona.

“Kuna wengine wanaingia kwenye hii mikopo ya kausha damu ambayo wanashindwa kuilipa kwa wakati na kusababisha sonona.”

“Madhara ya sonona  ni pamoja na muhusika kufikia hatua ya  kujiua kwa sababu akitafakari anakuta hana uwezo wa kulipa hilo deni,” amesema Dk Mwisomba.

Pia amesema ili mtu awe na afya nzuri ya akili ni lazima apate usingizi wa kutosha kati ya saa nane hadi tisa, ili kuuwezesha mwili kupumzika na akili.

“Kuna wengine unakuta wanachezea simu usiku kucha na asubuhi anatakiwa kazini hana hata muda wa kupumzika sasa mtu kama huyu ni lazima apate changamoto ya afya ya akili, kwa sababu mwili unatakiwa kupumzika na siyo kufanya kazi muda wote,” amesema.

Amesema njia nyingine ya kuwa na afya ya akili bora ni kwenda kuwaona wazazi hasa kwa wanaoishi mbali nao, kwani mawazo ya kuwakosa huwa yanaweza kusababisha ugonjwa wa akili.

Amesema kitu kingine ambacho mtu anatakiwa ajilinde ili asipate ugonjwa wa afya ya akili ni kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya ya aina yoyote, kwa sababu ndiyo chanzo cha matatizo ya afya ya akili.

Amesema kati ya wagonjwa 10 wanaolazwa katika Hospitali ya Mirembe, wanane kati yao wamegundulika kutumia dawa za kulevya kama vile bangi, vilevi, sigara, cocein, heroin, mirungi na aina nyingine.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Mirembe, Dk Paul Lawala amesema ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha kuwa watu ambao bado wana afya ya akili iliyo bora walindwe ili wasipate ugonjwa huo.

Amesema hata jamii inayowazunguka imekuwa na tabia ya kutoa matukio yaliyofanywa na wagonjwa wa afya ya akili, badala ya kulinda watu wasipate ugonjwa huo kwani unazuilika.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wagonjwa sugu wa afya ya akili ni asilimia moja, sonona huwa inampata mtu mmoja kati ya wanne sawa na asilimia 25 na kila baada ya sekunde 40 mtu mmoja hujiua kutokana na sababu ya magonjwa ya afya ya  akili.

Related Posts