Majaliwa awataka wananchi kujiepusha na mikopo umiza

Geita. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka wajasiriamali wadogo nchini, kutumia majengo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyojengwa kwenye baadhi ya Halmashauri kupata elimu ya kuanzisha biashara na kupata mikopo kwa riba nafuu, ili kuondokana na mikopo umiza.

Akizungumza leo Jumapili, Juni 2, 2024, Majaliwa amesema uwepo wa vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi, itawahamasisha kujiunga kwenye shughuli za kibiashara na kujipatia kipato.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akihutubia wananchi kwenye uwanja wa Sabasaba, Kata ya Kharumwa wilayani Nyang’hwale mkoani Geita.

Amesema ni  agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa halmashauri zote nchini kutenga maeneo  maalumu yenye tija kwa wafanyabiashara ili waweze kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na kujenga mazingira ya kiuchumi kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Kila mmoja anaweza kubuni biashara jengo hili litatoa elimu kwa wajasiriamali walioamua kufanya biashara, pale mtapata elimu ya namna ya kuanzisha biashara yako,  kutumia mtaji wako na kufuatiliwa mwenendo wa mkopo wako, anzisheni biashara milango iko wazi,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu pia amezindua mwongozo wa vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi, utakaotumika kwa mikoa yote ya Tanzania Bara.

Akizungumzia utendaji kwa watumishi wa umma, Majaliwa amewataka watumishi kutumia ofisi kwa siku chache za wiki kama sehemu ya kuratibu utendaji kazi na siku tatu hadi nne kuzitumia kwenda vijijini kukutana na wananchi.

“Nendeni vijijini kukutana na wananchi mkaangalie mahitaji ya maji, elimu utoaji huduma za afya hakuna sababu ya kukaa ofisini muda mrefu, sikilizeni kero na kuzitatua badala ya kusubiri ujio wa Rais au mawaziri wananchi waje wamebeba mabango ya kero zinazowakabili,” amesema.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa kituo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi Beng’i Issa amesema hatua hiyo  umetokana na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, inayotaka kuanzishwa kwa vituo vya uwezeshaji kiuchumi kwa kila mkoa ili kupeleka huduma kwa wananchi.

Amesema vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini kwa sasa vipo 20, huku vitatu vikiendelea kujengwa.

Amesema vituo hivyo vinatumika kurasimisha biashara, ushauri wa biashara, elimu na mafunzo ya ujasiriamali, upatikanaji wa teknolojia na ufundi elimu ya vikundi vya kifedha vya kijamii na uongezaji wa thamani wa bidhaa.

“Lengo la kuanzishwa kwa vikundi hivi ni kuwaondolea adha wajasiriamali, wakulima na wafanyabiashara wenye lengo la kupata huduma za mikopo masoko na kurasimisha biashara zao na kupata huduma kwenye jengo moja,” amesema Issa.

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande akizungumza kwenye mkutano huo amesema kipo kilio kikubwa kwa wananchi wanaoingia kwenye mikopo umiza, kutokana na kukosa elimu sahihi ya matumizi ya fedha na matumizi ya mkopo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela akizungumza kwenye mkutano huo amesema katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 486 vilivyopo.

Katika sekta ya madini kwa kipindi cha miaka mitatu mkoa wa kimadini wa Mbogwe wenye wilaya za Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale leseni 1,000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.

Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya, elimu na maji lengo likiwa ni kuwafikishia wananchi huduma karibu.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Husna Toni amesema uwepo wa kituo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi, sio tu kitawawezesha wajasiriamali kupata elimu bali pia kitawaondolea wafanyabiashara adha ya kusafiri zaidi ya kilomita 90 kwenda Geita kupata huduma ofisi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mkuu wa Wilaya hiyo, Grace Kingalame amesema miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Sh28 bilioni zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa  miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya, elimu, maji na utawala.

Related Posts