Sh999 bilioni zakusanywa uwekezaji ardhi Unguja, Pemba

 Unguja. Dola 384 milioni za Marekani (Sh999.6 bilioni) zimewekezwa katika visiwa vidogo vidogo Unguja na Pemba huku  Dola 20.5 milioni (Sh53.3 bilioni) tayari zimekusanywa zikiwa ni gharama ya uwekezaji ardhi. 

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mwaka 2021 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), iliruhusu uwekezaji wa visiwa vidogo vilivyopo Unguja na Pemba, kati ya visiwa 52, vilitangazwa 20 vya awali huku 17 kati ya hivyo vikiwa vimeshapa wawekezaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Jumapili Juni 2, 2024, mjini Unguja, Zanzibar, Katibu Mkuu Wizara Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Khamis Suleiman Mwalim amesema uwekezaji katika visiwa hivyo unakwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kuimarisha uwekezaji katika sekta ya uchumi wa buluu.

“Uwekezaji utakaofanyika katika visiwa hivi wananchi watafaidika kwa kupata ajira 7,000 na utaongeza ukuaji kwenye pato la Taifa kupitia kodi na mapato mengine yatakayokusanywa,” amesema.

Kutokana na uwekezaji huo, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi anatarajia kufungua mradi wa kwanza wa uwekezaji katika Kisiwa cha Bawe. 

Mradi huo unaojulikana Bawe Island unamilikiwa na wawekezaji wa kigeni kutoka Italia kwa gharama ya Dola milioni 37 za Marekeni (Sh96 bilioni) ukitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 400. 

Katika kuzingatia umuhimu wa kutunza bahari na mazingira katika uwekezaji wa visiwa hivyo, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Usiad Heshimu Bahari, imeandaa kongamano la kuhifadhi bahari litakalofanyika Julai 11 ili kuhakikisha wawekezaji wote waliopata fursa hiyo kutunza mazingira ya bahari.

Wakati huohuo, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema miradi ya uwekezaji katika sekta ya hoteli inafikia 260 na asilimia 70 ipo katika sekta ya utalii hususani katika ujenzi wa hoteli kubwa.

Ametoa kauli hiyo wakati akizindua ujenzi wa hoteli ya nyota tano ya Azure Michanvi Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema uwekezaji huo una maana kubwa katika jamii na Taifa kwa sababu unachochea ukuaji wa uchumi na kustawisha jamii.

“Hoteli kama hizi zitaunganisha moja kwa moja na mnyororo wa thamani kwa wananchi, watakaouza mazao yao hapa lakini  kuwa chachu ya kuifungua Zanzibar,” amesema Ramadhan.

Amesema wataendelea kuweka miongozo na kanuni ili kutoa fursa kwa wazawa.

Mwekezaji wa mradi huo, Simon Nikitas amesema mradi huo wa Dola 10 milioni za Marekani (Sh26 bilioni) unajumuisha majengo ya kifahari 54 mengine yakiwa juu ya maji na ufukwe wa bahari.

“Sisi tumehamasika kuwekeza Zanzibar kutokana na utulivu, mandhari nzuri na mazingira yake kwa jumla,” amesema Ramadhan. 

Baadhi ya wananchi wa eneo hilo walitaka kupewa vipaumbele wakati wa ujenzi wa mradi huo utakapokamilika.

“Tunachoomba tupewe vipaumbele kufanya kazi hapa na itakapokamilika vijana wetu waajiriwe,” amesema Sheha wa Shehia ya Michanvi Hadija Hassa Haji.

Related Posts