KLABU ya Simba Queens imeanza kufuatilia kwa ukaribu dili la beki wa kati wa Wiyeta FC ya Kenya, Lorine Ilavonga (17) katika mipango ya kufanya maboresho eneo la ulinzi kuelekea msimu ujao.
Inaelezwa beki huyo ambaye mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu anahitajika na klabu mbalimbali ikiwemo Police Bullets ya nchini Kenya.
Beki huyo kinda anatazamwa kuwa mbadala wa Ruth Ingosi na Daniela Ngoyi ambao wamekuwa wakipata nafasi chache ya kucheza kutokana na ubora wa wazawa Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus.
Mmoja wa wasimamizi wa mchezaji huyo (hakutaka jina liandikwe) alisema ni kweli wamepokea ofa kutoka klabu mbalimbali ikiwemo Tanzania.
“Kuna timu zimeleta ofa zinamuhitaji ikiwemo Simba kwa hivyo tunaangalia ofa nzuri na uwezekano wa mchezaji kucheza ingawa Tanzania kuna fursa zote za kifedha na hata nafasi kutokana na ligi hiyo kukua sana,” alisema.
Alipotafutwa Meneja wa Simba Queens, Selemani Makanya alisema: “Hizo ni tetesi tu watu wasubiri kwanza tumalize msimu halafu tutajua.”