Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kupitia mradi Jumuishi kati ya wasindikaji na wazalishaji wa Maziwa (TI3P), unaotekelezwa na benki hiyo ikishirikiana na Heifer International na Land o Lakes, imetoa mikopo yenye thamani ya bilioni 26 katika sekta ya maziwa.
Hayo yameelezwa leo na Meneja wa Kanda TADB, Alphonce Mokoki, wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti alipotembelea banda la benki hiyo leo kabla ya kufunga maadhimisho ya wiki ya maziwa kitaifa yaliyofanyika jijini Mwanza.
Amesema hadi sasa TADB kupitia mradi huo imetoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 26,imewafikia wafugaji 69,062 kati yao asilimia 30 ni wanawake,vyama vya ushirika 45, viwanda sita na wametoa mkopo wa ng’ombe wa kisasa 1,748 kwa wafugaji.
Pia kupitia huo mradi wametoa ruzuku ya sh.milioni 738 kwa wafugaji 846 lengo likiwa na kuwainua kiuchumi kupitia ufugaji bora wa ng’ombe wa kisasa wenye tija katika uzalishaji wa maziwa.
Naye Ofisa Programu wa Heifer International,Nyamate Musobi,amesema kupitia mradi huo Jumuishi kati ya wasindikaji na wazalishaji wa Maziwa (TI3P), wamewafikia watu zaidi ya 20,000, vikundi 960 na vyama vya ushirika 45 Kanda ya Ziwa
Amesema mradi huo umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2022 hadi Juni 2024,lengo kuu ni kuwawezesha wafugaji kuongeza kipato kitokanacho na uzalishaji wa maziwa ili kufikia lengo hilo kuu, mradi una malengo mengine mahsusi manne.
“Malengo ni kuongeza uzalishaji endelevu wa maziwa, kuongeza ubora wa maziwa,kuimarisha miundo mbinu ya ukusanyaji maziwa na vikundi (vyama) vya wazalishaji,kuelimisha wafugaji masuala ya jinsia na lishe, hivyo kuongeza uwiano wa kijinsia katika mnyororo wa thamani wa maziwa na ujumuishaji wa masuala ya lishe,”amesema Musobi.
Ofisa Ofisa Programu wa Heifer International,Nyamate Musobi (kushoto),leo akimweleza Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (wa pili kulia),kuhusiana na kuongeza ushiriki wa wanawake katika mnyororo wa thamani ya maziwa,wa pili kushoto ni Msajili ya Bodi ya Maziwa, Profesa George Msalya
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti (wa pili kulia),akimuuliza jambo Ofisa Programu wa Heifer International,Nyamate Musobi (kushoto),leo alipokagua banda la shirika hilo lisilo la kiserikali kabla ya kufunga maadhimisho ya wiki ya maziwa kitaifa, jijini Mwanza.Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Izara hiyo, Profesa Daniel Mushi.
Picha zote na Baltazar Mashaka