Wakati Kamati ya Uchaguzi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika Law Society (TLS) ikiongeza muda kwa wanachama zaidi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, wakili Boniface Mwabukusi ajitosa kuwania urais, huku mwenyekiti wa AYL anayemaliza muda wake Edward Heche akieleza kuwa hatogombea tena.
Chama hicho kinatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Agosti 2, 2024, jijini Dodoma, kuwapata viongozi wapya watakaokiongoza katika nafasi mbalimbali zikiwamo za rais, makamu, mhazini na wadhamini wa mifuko ya chama hicho na wawakilishi wa kamati ndani na nje ya chama hicho.
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Nelson Frank alilieleza Mwananchi kuwa uchaguzi wa viongozi kwa nafasi hizo za juu utatanguliwa na uchaguzi wa mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Vijana ( Young Lawyers Associatio – YLA) na viongozi wa Kanda za chama.
Uchaguzi wa viongozi hao ambao ni wajumbe wa Baraza la Uongozi TLS (Governing Council – GC), utakaofanyika Julai 31, 2024.
Lakini kwa upande wa nafasi ya mwenyekiti wa AYL iliyokuwa inashikiliwa na Wakili Edward Heche ambaye amemaliza muda wake baada ya kuitumikia kwa vipindi viwili.
Katika nafasi hiyo wagombea waliojitokeza kumrithi Heche ni Emmanuel Phales Ukashu (Ilala), Victor Kweka (Dodoma), Karangi Joel Karangi (Kinondoni), Joseph Gidion Lameck (Kinondoni) na Moses Matiko Misiwa (Mwanza).
Heche amelieleza Mwananchi kuwa baada ya kumaliza muda wake wa uongozi kwenye nafasi ya AYL, katika uchaguzi huo hatagombea nafasi nyingine yoyote ndani ya TLS, bali ameamua kupumzika huku akiwashukuru mawakili vijana kwa kumuamini kuwaongoza katika vipindi vyote na kwa ushirikiano mzuri waliompatia.
Amesema kuwa katika kipindi ambacho amekiongoza chama hicho kwa kushirikiana na wanachama wameweza kufanya mambo mengi, ikiwa ni pamoja na kupaza sauti kutetea masilahi ya mawakili vijana ndani na nje ya chama na kuiimarisha zaidi TLS.
“Baada ya muda huu wa vipindi viwili, kwa kuwa mimi ni muumini wa demokrasia nina imani watakuja viongozi wapya, watakaoleta mawazo mapya zaidi wa kukipeleka mbele chama kuanzia hapo nilipoishia”, amesema Heche na kuongeza.
“Sitagombea nafasi yoyote hata ndani ya TLS kwa sasa bali mahitaji kupumzika kwanza na kuona wengine wanafanya nini kuijenga TLS.”