Arusha. Wananchi wameendelea kung’ang’ania kipengele cha kupunguza madaraka ya Rais kiwekwe kwenye Rasimu ya Katiba Mpya ikiwemo uwezo wa kuteua wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa halmashauri. Wakitaka nafasi hizo ziombwe na wasomi waliopo nchini kupitia ofisi ya Tamisemi.
Mbali na hilo, wamesema kuwa Rais aondolewe uwezo wa nafasi 10 za kuteua wabunge, Katibu wa Bunge na pia asiweze kulivunja Bunge kwa sababu yoyote ile.
Maoni hayo yametolewa leo Jumapili Juni 2, 2024 jijini Arusha, kwenye mdahalo wa wazi wa wadau wa masuala ya kisheria, viongozi wa asasi za kiraia na wanafunzi wa vyuo vya kisheria ulioandaliwa na Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Wakizungumza kwenye mdahalo huo, wamesema kuwa madaraka ya Rais yanayompa uwezo wa kuteua baadhi ya watendaji serikalini, imekuwa chanzo cha kutumikia yale anayoyapenda (aliyewateua) hata kama yako kinyume na wananchi.
Mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, Ester Maro ambae ni mwanafunzi wa masuala ya sheria Chuo Kikuu cha Sauti, amesema kuwa wako wasomi wengi nchi hii wenye uwezo mkubwa wa kutumikia wananchi watakapopewa nafasi, kuliko wanaoteuliwa wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika matokeo yake wanakwenda kutumikia wananchi kwa Ilani ya chama, wakilenga kumfurahisha bosi wao aliyewateua.
“Ingependeza pia asiwe Mwenyekiti wa chama chake alichopita, bali awe mwanachama wa kawaida na mwenyekiti awe mtu mwingine ili kutoa nafasi ya kukosolewa hata na wabunge wa chama chake pindi anapokosea, kuliko kusifiwa kila kukicha kwa sababu ni bosi, ” amesema Ester.
Naye Wakili Mwandamizi, Alute Mughwai amesema ingependeza mchakato huo wa kupata Katiba Mpya, Rais asishiriki ili kutoa nafasi ya maoni mengi yatakayoonekana yanafaa kupita bila kupingwa ikiwemo yale yatakayomgusa moja kwa moja.
“Kwa mfano hii kauli ya mitano tena inayotamkwa na kila mtu, inaweza kuwa na madhara makubwa mbeleni isipojadiliwa na kupatikana Katiba Mpya yenye mwongozo wa uchaguzi, kabla ya uchaguzi wenyewe ujao wa wabunge na Rais” amesema Mughwai.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Asasi ya kiraia ya Angonet, Peter Bayo amesema kuwa tatizo la Katiba ya sasa inaacha mianya mingi inayolenga kumuwekea ulinzi Rais asishtakiwe hata kama ataonekana kafanya kosa kubwa kiasi gani.
“Katiba iruhusu Rais ashtakiwe, lakini pia akishinda uchaguzi kwenye njia ambazo wananchi hatuelewi ni bora kuwe na kipengele cha matokeo kupingwa mahakamani, hii itaongeza uwazi na wajibikaji mwema kwenye nafasi yake,” amesema Bayo.
Awali akizungumzia mdahalo huo, Mwenyekiti wa Mawakili kanda ya kaskazini, David Shilatu amesema lengo lake ni kutoa elimu kupitia TLS kuhusiana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
“Katiba tuliyonayo ni ya mwaka 1977, hapa tunazungumzia zaidi ya miaka 47, lakini imefanyiwa mabadiliko zaidi ya mara 14, nadhani unapata picha mkataba huu wa wananchi na watawala ulivyopitwa na wakati, ndio maana tunatoa elimu hii ili wananchi watoe maoni na tutaenda kuyapitisha kwenye mikutano yetu na kuwa ndio maoni ya chama chetu,” amesema Shilatu.
Amesema, kadri upatikanaji wa fedha utakapowaruhusu, wanalenga kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni hayo ya wananchi, kuanzia katika masoko, vijiwe vya kahawa, mitaani na hata kwenye taasisi za elimu ili kupata mawazo mapana zaidi.
Naye Wakili wa kujitegemea, Francis Stolla amesema kuwa katiba ikipatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao, itakwenda kuijengea nchi heshima kubwa bila kujali itakuwa na vitanzi vya aina gani ndani yake ili mradi imetokana na maoni ya wananchi.
“Hadi sasa wananchi wanatamani mchakato uanze upya na wengi wakisisitiza madaraka ya Rais yapunguzwe, lakini wabunge wawe wanapimwa kwa kazi zao ili kuwa na sifa ya kukaa madarakani,” amesema Wakili Stolla.