Unguja. Wizara ya Afya imeainisha vipaumbele 10 itakavyotekeleza katika bajeti ya mwaka 2024/25 ikiwamo kupunguza vifo vya mama wajawazito kutoka vifo 145 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mwa 2023/2024 na kufika vifo 123 kwa kila vizazi hai 100,000.
Kadhalika, kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka vifo 28 kwa kila vizazi hai 1000 na kufikia vifo 26 kwa kila vizazi hai 1000.
Kwa mujibu wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, lengo ni kufikia vifo 12 kwa kila vizazi hai 1000 ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 3, 2024 na Waziri wa Afya, Ahmed Nassor Mazrui wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 katika Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja.
Ametaja vipaumbele vingine ni kuimarisha miundombinu ya afya katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya, ikiwemo matengenezo ya majengo na vyombo vya usafiri.
“Kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, kuimarisha mifumo ya kidijitali ya taarifa za afya, kuimarisha ubora wa utoaji wa huduma za afya kwa kuajiri wataalamu wenye sifa na kupeleka masomoni madaktari na wafanyakazi wa kada nyingine za afya,” amesema waziri huyo.
Vingine ni kuimarisha mifumo endelevu ya kugharamia huduma za afya ikiwemo mfuko wa afya Zanzibar, kuimarisha huduma za afya ya msingi kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Hospitali ya Mnazimmoja
Amesema Hospitali ya Mnazi mmoja inalenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi kwa wagonjwa kwa ushirikiano na sekta binafsi pamoja na upatikanaji wa huduma za matibabu ya rufaa.
Kadhalika itaendelea kutoa huduma za kibingwa ikiwemo usafishaji damu kwa wagonjwa zikiwemo huduma za figo, uchunguzi wa saratani, matibabu ya satarani, huduma za ubongo na uti wa mgongo
Kuanza ukarabati na utanuzi wa Hospitali ya Mnazimmoja kupitia mradi wa BADEA, Saudia na Kuwait.
Kwa mujibu wa waziri, Mshauri elekezi ameshaanza kazi alizopangiwa ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu, michoro na makadirio ya gharama za ukarabati wa majengo ya zamani na ujenzi wa majengo mapya.
Amesema mradi upo kwenye hatua ya kutafuta mkandarasi na zabuni imeshatangazwa na wazabuni wanaendelea kuwasilisha maombi ya ujenzi.
Ili kuhakikisha kwamba huduma za uchunguzi na matibabu zinaimarika zaidi, Wizara imetenga Sh142.2 bilioni sawa na asilimia 50 kati ya hizo Sh136.3 bilioni kwa ajili ya programu ya matibabu na Sh5.9 bilioni kwa ajili ya programu ya uchunguzi.
Amesema wamejipanga kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu katika hospitali za wilaya na mkoa, kutekeleza mfumo wa rufaa kwa wagonjwa katika ngazi zote za utoaji wa huduma.
Waziri Mazrui amesema huduma za matibabu ya kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, zimeendelea kutolewa kwa wagonjwa 540 wakiwemo wagonjwa wapya 71.
Pia, wagonjwa 204 wanapatiwa huduma katika kliniki ya saratani.
Katika hatua nyingine, wagonjwa 5,225 wamepatiwa matibabu katika kliniki maalumu ya maradhi ya moyo, ambapo wagonjwa 1,267 ni wapya na wagonjwa 3,958 wa marejeo.
Mwenyekiti wa kamati ya Ustawi wa Jamii, Sabiha Filfil Thani, amesema miongoni mwa njia moja wapo ya kuiongezea mapato Serikali ni kusajili vituo vya afya vilivyopo nchini.
Hivyo imeshauri wizara kuwa na utaratibu wa kuvifuatilia na kuvisajili vituo ambavyo bado havijasajiliwa hususani vituo binafsi vinavyotoa huduma za matibabu ya afya vilivyopo hotelini, kwani imebaini kuwa kumekuwa na vituo vingi ambavyo vikipatiwa utaratibu na kusajiliwa vitaongeza mapato serikalini.
Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema bado kuna changamoto ya madaktari bingwa katika hospitali za wilaya, kwani mgonjwa anaweza kwenda kupata huduma kuanzia saa 12:00 asubuhi akarudi saa 2:00 usiku.
“Wataalamu wapelekwe katika hospitali za wilaya wasaidiane na waliopo kuokoa jahazi na katika hospitali hizi tunahitaji kuwa na vifaa tiba, maana ngazi ya wilaya ni hospitali muhimu,” amesema.
Aza Januri Joseph, mwakilishi viti malumu, amesema wizara inajitahidi kupiga hatua kutokomeza magonjwa ya ukimwi na homa ya ini lakini bado kunaendelea kujitokeza tatizo hilo.
Ameitaka wizara kutoa ufafanuzi kuhusu elimu inayotolewa kama walengwa wanaipata na kufanya tathamini ya elimu wanayopata kama inatosha.
Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad, amesema kila bajeti mambo yanakuwa yaleyale kwani kila wakati wanasema hakuna wataalamu ilhali afya haiwezi kusubiri.
Amesema kinachokosekana ni usimamizi thabiti wa watendaji wa wizara hivyo na hivyo kusababisha changamoto hizo.
“Afya ni wataalamu na sio majengo, tunataka kujua tunapoelekea lakini bado huduma zinapwaya,” amesema.
Naye, mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu, amesema kuna haja ya kuimarisha mifumo ya Tehama ili kurahisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
“Bila kufanya hivyo tutashindwa kupata wataalamu lakini tukitumia mifumo hiyo mgonjwa atatibiwa akiwa alipo na itapunguza shida ya kukosa wataalamu,” amesema.
Mwakilishi wa Paje Dk Soud Nahoda Hassan, kwa upande wake, ametaka uimarishaji wa bima ya afya ili kuongeza ufanisi katika hospitali za wilaya.