Njombe. Jana, katika simulizi hii katekista Daniel Mwalango au ‘Dani’ alipanga na kutekeleza mauaji Nickson Myamba kisha akaanza kutumia simu ya marehemu, kutuma ujumbe (SMS) kwa mkewe na kiongozi mwingine wa kanisa akijifanya ndiye Myamba.
Makala haya yanaegemea hukumu iliyotolewa Desemba 12, 2023 na Jaji Said Kalunde wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, baada ya kusikiliza ushahidi uliomtia hatiani mshitakiwa na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
SMS hizo hazikuishia tu kutumwa kwa mke wa marehemu, bali kwa viongozi wengine wa kanisa zikieleza katekista (Myamba) amepata ajali wakati anarudi nyumbani na anaelekea hospitali.
Hata hivyo, SMS hazikueleza anaelekea hospitali gani, ndipo mkewe na viongozi wa kanisa wakaamua kuanzia Kituo cha Polisi Makambako walikoelezwa kuwa, hapakuwa na taarifa yoyote ya ajali. Sasa endelea.
Katekista alivyogoma kutoa ushirikiano
Baada ya mkewe na viongozi wengine wa kanisa kumtafuta Myamba kituo cha polisi na hospitali bila mafanikio, shahidi wa pili, Michael Mwiluka alijaribu kumpigia simu Dani ili kumuuliza juu ya mahali alipo Myamba.
Alimtaka Dani afike parokiani wasaidiane kumtafuta Myamba kwa sababu kuna taarifa amepata ajali, lakini kwa mshangao, Dani aliyekuwa anakaa umbali wa mita 300 au 400 kutoka kanisani hapo, alikataa.
Akawaambia angependa kuungana nao kumtafuta lakini kwa muda ule ulikuwa tayari ni usiku na kwa maneno yake alisema alimnukuu; “Ningependa kuja lakini ni usiku.”
Katibu wa Parokia ya Makambako, Moses Lubangula ambaye naye alikuwa amefika kuungana na mke wa Myamba na viongozi wengine, aliamua kuendesha gari lake hadi nyumbani kwa Dani, ili kwenda kumchukua ashiriki kazi hiyo.
Alipofika nyumbani kwa Dani, hakuwepo na walipompigia, aliwaambia kuwa tayari yuko njiani kwa mguu kwenda kwenye kigango, kupitia njia ya makaburini, lakini hata hivyo hakufika na kuwaweka viongozi hao katika wakati mgumu.
Mbunge ‘Jah Pipo’ alivyokoleza utafutaji
Myamba amepotea na Dani anagoma kutoa ushirikiano, viongozi wa kanisa hawakuwa na njia nyingine zaidi ya kutoa taarifa tena Polisi Makambako na wakaomba pia msaada kwa mbunge wa Makambako, Deo Sanga maarufu Jah Pipo.
Mbunge huyo akaomba kuongezewa nguvu kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi (OC-CID) Wilaya ya Makambako, Josam Gabikwa aliyeelekeza gari la doria liwasindikize viongozi wa kanisa na mkewe Nickson hadi nyumbani kwa Dani.
Hata hivyo, Dani hakuwepo tena, hapo ndipo polisi wa doria, viongozi wa kanisa na mke wa Myamba wakaamua kurudi kanisani kufanya uchunguzi.
Mwili wagundulika kwenye sandarusi
Waliporudi kanisani, walihitimisha ukaguzi wao kwenye duka la vitabu walikobaini uwepo wa matone ya damu karibu na duka hilo.
Katika hali ya kushtua, kulionekana kinyunyizio cha mkono kikiwa na damu nje ya mlango.
Taarifa hiyo ilipelekwa kwa OC-CD, Josam Gabikwa aliyekuwa shahidi wa sita, ambaye alifika kanisani kuungana na watu wengine, kujua nini kilikuwapo nyuma ya ule mlango.
Mlango ulikuwa umefungwa kwa kufuli la Solex, na baada ya kupata ridhaa kutoka kwa paroko ya kuvunja mlango, walipoingia ndani, walishtuka kuona mwili wa Myamba ukiwa umetenganisha vipande viwili.
Mifuko ya nailoni iliyokuwa na vipande hivyo vya mwili wa Myamba ilikuwa imewekwa ndani ya mifuko ya sandarusi na mfuko mmoja ukiwa na mwili wa katibu huyo wa Kigango cha Makambako, uliwekwa kwenye boksi.
Baada ya mwili huo kutambuliwa, ulipelekwa chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Nazareth, lakini siku iliyofuata saa 2:00 asubuhi, timu ya makachero ilirudi tena eneo la tukio na kubaini ndoo iliyokuwa na damu, pembeni yake polisi walipata majoho na nguo moja zikiwa na damu.
Nguo hizo ndizo zilitumika kusafisha duka baada ya mauaji, pia walipata mifuko miwili ya nailoni kati ya minne na miwili ni ile iliyotumika kuficha mwili wa marehemu.
Uchunguzi ulihamia nyumbani kwa Dani, katika upekuzi, ilipatikana suruali ya rangi ya kijivu ikiwa katika chumba cha kulala cha Dani huku ikiwa na matone ya damu. Suruali hiyo ikachukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi.
Katekista alivyodakwa na kusimulia kila kitu
Wakati mambo yote hayo yakitokea, katekista Dani alikuwa amefanikiwa kutoroka kuelekea Dar es Salaam lakini hata hivyo saa 4:00 usiku wa Februari 10, 2022 eneo la Doma, Wilaya ya Mvomero Morogoro, alikamatwa na polisi.
Alisafirishwa hadi Kituo cha Polisi Morogoro na alikofikishwa usiku wa kuamkia Februari 11 2022.
Shahidi wa tatu, Inspekta John Mapuga, alielekezwa na Mkuu wa Upelelezi (RCO), Morogoro kwenda kumchukua mtuhumiwa huyo.
Inspekta Mapuga alimchukua Dani na kumpeleka Kituo cha Polisi Makambako na kumkabidhi.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Francis Ngatunga aliyekuwa shahidi wa 11 alirekodi maelezo ya onyo ya mshitakiwa na yalitolewa kama kielelezo.
Ombi la kuomba maelezo hayo yapokewe kama kielelezo halikupingwa na Mahakama, hivyo yalipokewa kama kielelezo P17 na katika mahojiano hayo, mtuhumiwa (wakati huo) alikiri kufanya mauaji hayo na kusimulia hatua kwa hatua.
Mbali na kukiri kufanya mauaji hayo, mshitakiwa alikubali kuwapeleka polisi hadi eneo alilokuwa ameficha silaha aliyoitumia kufanya mauaji na kipande cha bomba kilipatikana ndani ya bomba kubwa au PVC.
Akawapeleka pia, Shule ya Msingi Makambako ambako ndani ya choo cha walimu wa kiume, kulipatikana panga lililotumika kutenganisha mwili wa Myamba.
Vielelezo hivyo na vilivyopatikana siku ya kwanza ikiwamo suruali iliyokutwa nyumbani kwa mshitakiwa, vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kupimwa vinasaba na kuoana na sampuli za mshitakiwa.
Katekista alivyosimulia mwanzo mwisho
Katika maelezo yake ya onyo aliyoyaandika polisi, katekista Dani alieleza hatua kwa hatua tangu alipoanza kuandaa vifaa vya kutekeleza mauaji.
“Nakumbuka mnamo tarehe 09/01/2022 kulikuwa na mkutano wa Kigango cha Makambako, katika kikao hicho kiliazimia kufanya mabadiliko ya muuza duka la kigango, mimi nilitakiwa kukabidhi kwa mtu mwingine.
“Nilitakiwa kukabidhi baada ya kukamilisha mahesabu ya vitu vyote na pesa; na baada ya hapo atatafutwa muuza duka mwingine. Mabadiliko hayo yalifanywa kwa sababu mimi nilikuwa sifungui duka muda wote, walitaka atakayefungua muda wote.”
“Nakumbuka viongozi waliokuwa wanafuatilia nikabidhi duka ni katibu wa kigango Nickson Myamba na mwenyekiti ndugu Michael Kihaga lakini mtu ambaye alikuwa akinifuata fuata mara kwa mara ni Nickson Myamba.”
Katika simulizi hiyo, Dani alieleza kuwa alieleza kuwa Februari 7, 2022, walikubaliana na Myamba kukutana ndani ya duka na wakiwa ndani ya duka, alisubiri hadi marehemu awe ‘busy’ kukagua hesabu ndipo atekeleze mauaji.
Usikose sehemu ya tatu kesho tukiwaletea neno kwa neno alivyosimulia Katekista Dani namna alivyoua na kutenganisha mwili wa marehemu vipande viwili, kudeki chumba na kuhifadhi mwili kwenye mfuko wa Sandarusi.
Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kupata mwendelezo wa simulizi hii kwa kina.