Mahujaji 3,300 wanaoenda kuhiji wapewa somo

Dar es Salaam. Mahujaji wanaokwenda kuhiji Makka  wametakiwa kuwa makini na kufuata maelekezo ya viongozi ili kunufaika na nguzo hiyo muhimu kati ya tano za kiislamu.

Pia, wametakiwa watakapokuwa hijja kujikita katika ibada kwa ajili ya mwenyezi Mungu.

Wito huo umetolewa leo Jumatatu Juni 3, 2024 na Sheikh Hamid Jongo kwa niaba ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir wakati wa hafla ya kuwaaga mahujaji kwa mwaka 2024 kutoka Umoja wa Taasisi za Hijja Tanzania Bara.

Jumla ya mahujaji 3,300  kutoka taasisi 13 za Hijja Tanzania Bara wanatarajia kuondoka nchini kwa nyakati tofauti kwenda Makka nchini Saudi Arabia kutekeleza ibada ya hijja.

 Shekh Jongo amesema kwa uzoefu wake endapo mahujaji watakuwa hodari wa kuwafuatilia wanaowaongoza kipi cha kufanya na kipi cha kuacha watakaporudi watakuwa kama watoto wachanga.

 “Ukiondoka kambini bila kuaga kutokana na majengo kunaweza kukuchanganya, unapotoka toa taarifa unakokwenda, unapokatazwa msikillize kiongozi wako huo ndio utaratibu,” amesema.

Aidha Sheikh Jongo amewataka wote watakaoenda hijja kuziacha familia zao vizuri kisaikolojia na kuwatoa wasiwasi.

Mwenyekiti kutoka Taasisi ya Jamarat, Shekh Mussa Kundecha amesema hijja ni nguzo moja kati ya nguzo tano za kiislamu.

Amebainisha kuwa fursa hiyo sio jambo la kukosa kwa kuwa mtu anapokwenda hijja anaporudi anakuwa mpya.

 “Jambo hili huwa linaharibika, mtu anapofika kule huanzisha mijadala tofauti na kusababisha kuharibu dhana nzima ya kile kilichompeleka,”amesema Sheikh Kundecha.

 “Hatutegemei kiongozi wa taasisi fulani anapoona hujaji kutoka taasisi fulani kapata tatizo akamuacha, mnapokuwa kule suala la huyu ni taasisi fulani na huyu taasisi hii ondoeni fikra hizo,” amesema.

Mwenyekiti wa Taasisi ya I Travel Sheikh Twaha Seleman amewataka mahujaji watakapokuwa hijja kupambana kikamilifu kuhakikisha wanasoma Quraan na hawakosi swala ili wanaporejea nchini wawe wamebadilika.

 “Itumieni fursa unapofika Makka, kama tutatumia fursa vizuri tutabadilika na hijja itakuwa na manufaa, wajibika na hiyo hijja yako tekeleza ibada kwa manufaa ya kidunia na akhera utajifunza mengi na kujuana na wengi,” amesema.

Mkurugenzi wa Mambo ya Hijja, Haidary Kambwili amesema umoja huo umeanzishwa mwaka huu kwa lengo la mahujaji kupata huduma zilizo bora na kuondoa changamoto zinazowakabili wanapokuwa hijja.

Amesema baada ya kuanzishwa kwa umoja huo, idadi ya mahujaji imeongezeka ikilinganishwa na miaka mingine.

 “Tanzania mwaka huu tulipewa nafasi za mahujaji 25,000 lakini idadi ya wanaoondoka ni 3,300 pamoja na kuwa hatujafikisha idadi hiyo lakini kwa mwaka huu imeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma,” amesema Kambwili.

Related Posts