Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha (RC), Paul Makonda amesema kuanzia sasa hadi Januari 1, 2025 atakuwa amekamilisha kazi ya kuwanyoosha watumishi wa umma wasiokuwa wazalendo na wanaotanguliza masilahi yao binafsi.
Makonda amemwomba Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi kwenda kumwombea kwa Rais Samia Suluhu Hassan amvumilie kwa kipindi hiki cha miezi sita akiwa anaifanya kazi hiyo.
Amesema hayo leo Jumatatu, Juni 3, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Dk Nchimbi uliofanyika soko la Kilombero, Arusha Mjini.
Amesema lengo ni kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, kusikiliza kero na kuangazia maandalizi ya chaguzi zijazo na ikifika Januari 1, 2025 atakuwa amekamilisha kazi na kama kutakuwa na mkoa mwingine yuko tayari kupelekwa.
“Nikuhakikishie katibu mkuu, watakula spana za kutosha.
“Nimekuta mkoa huo kuna watumishi wasiokuwa wazalendo, hawataki kujituma, sio wote ila wengi wao wanatumia masilahi yao binafsi, naomba kaniombee kwa Rais, anivumilie kidogo, mfunge masikio nipige spana ili haki za wananchi zipatikane.
“Nitawanyoosha mpaka kieleweke na ikifika Januari 1, 2025 utakuwa mkoa wa mfano,” amesema.
Amesema kuna zaidi ya Sh20 bilioni ambazo zinaweza kurudi serikalini kutokana na kutolewa ili kutekeleza miradi mbalimbali, lakini hazijatumika pasina sababu za msingi huku wananchi wakilia kukosa huduma za afya, maji na elimu na hayuko tayari kuona hilo likitokea.
Hivi karibuni, Makonda alifanya ziara katika wilaya zote za mkoa huo, kukagua miradi mbalimbali za maendeleo na katika ziara hizo, mkuu huyo wa mkoa aliyefikisha mwezi mmoja na wiki kama mbili alichukua hatua kadhaa kwa watumishi.
Wabunge waeleza mafanikio, kero
Katika salamu zao, wabunge wa mkoa huo wameeleza mafanikio na changamoto kwenye majimbo yao.
Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangay amesema wilaya hiyo tangu Uhuru haijawahi kwenda upinzani na mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu karibu wilaya zote za Arusha zilikwenda upinzani.
Shangay amesema wilaya hiyo haijaunganishwa na Arusha kwa barabara, suala jingine ni uharibifu wa barabara uliotokana na mvua.
“Maeneo mengi ya wilaya hiyo kuna shida ya maji. Tunaomba katibu mkuu ulifanyie kazi. Tatizo jingine ni maeneo ya malisho hasa baada ya eneo kutengwa. Mwaka jana ng’ombe zaidi ya 16,000 zilitaifishwa kutokana na kutokuwa na malisho,” amesema Shangay.
Naye Mbunge wa Arumeru Mashariki, Dk John Pallangyo amesema tunashida kubwa sana ya barabara na mbaya zaidi tuna ahadi ya Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, ahadi hiyo haijatekelezwa.
“Kilomita tano pale Usa River ya Hayati Magufuli haijatekelezwa, pia Kikatiti kwenda Sakira ya Waziri Mkuu nayo haijatelelezwa. Hizi ahadi zinatutafuna. Tunaomba upeleke juu ziweze kutatuliwa,” amesema Dk Pallangyo.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amesema kuna soko jipya na la kisasi linajengwa Kilombero, lakini matokeo ya safari hizo za Rais Samia zimewezesha kupatikana fedha za ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, ujenzi wa barabara, elimu na afya.
Gambo amesema Hospitali ya Maunt Meru imepelekewa vifaa mbalimbali na huduma kwa sasa zinatolewa eneo hilo na wananchi kupunguziwa adha.
Gambo aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kwenye mafanikio hakukosi changamoto na anapozungumzia changamoto watendaji wa Serikali wanapaswa kuwa wanamwelewa.
“Mimi nikiwa mwakilishi wa jimbo hili, tangu mkuu wa mkoa amekuwa Makonda ninalala usingizi, Makonda anapopiga spana inasaidia kwani bila hivyo chama chetu kitapata shida,” amesema Gambo.
Amesema sisi wananchi wa Arusha Mjini, licha ya utalii tunategemea madini, lakini kwa sasa madini ya Tanzanite hayauzwi Arusha hivyo zaidi ya vijana 3,000 wamekosa ajira na Serikalini ameelezwa kuna taratibu zinaandaliwa kurejesha soko hilo hivyo kamwomba Dk Nchimbi kupeleka msukumo zaidi.
Pia, amesema tulikuwa na changamoto ya machinga, maekelezo ya Rais tuwapange vizuri, lakini baadhi ya watendaji walitumia vibaya, waliwapiga na kuwapora na kumwomba Makonda kusimamia hilo.
Gambo amesema kuna changamoto kubwa pale Soko la Kilombero, nilipochaguliwa kuwa mbunge tulichimba kisima lakini watendaji wa Serikali wameshindwa kukisimamia. Sasa sijui wanafanya kazi gani.
Mbunge wa Longido ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema mambo mengi ya maendeleo yamefanyika na changamoto ya malisho na mipaka ni ndogondogo ambazo tunaweza kuzifanyia kazi.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Lembris amesema kuna changamoto ya barabara kutokana na mvua lakini Serikali imetoa fedha kujenga ikiwamo ya Mianzini kwenda Kimboro hadi Ngara Mtoni inajengwa.
“Changamoto ni nyingi, tutawasilisha bungeni, mkuu wa mkoa (Paul Makonda) yupo na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa (Thomas Ole Sabaya) wapo watazifanyia kazi,” amesema.
Katika mkutano huo, Dk Nchimbi amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani Machi 19, 2021 wapo waliosema hatoweza lakini kwa alichokifanya mpaka sasa ameonesha mwanamke anaweza na amefanya kazi kubwa.
Dk Nchimbi amewasisitiza Watanzania kuendeleza ushirikiano na kukemea vitendo vya mgawanyo unaoelezwa na watu na hilo ni jukumu la kila mmoja kutetea Muungano na kudumisha umoja wa Kitaifa.
Mtendaji mkuu huyo wa chama amesema viongozi wa chama na Serikali mkoani humo wanajitahidi kutimiza wajibu wao ipasavyo na wanapaswa kuendeleza juhudi hizo.
“Kero za wananchi ni sehemu muhimu ya kutekeleza majibu yetu ya kila siku, kiongozi hapaswi kukimbia kero, atumia njia zote kuzitatua na kama ameshindwa amweleze nguvu zangu zimeisha hapa,” amesema Dk Nchimbi.
Kuhusu kero ya uuzwaji wa madini, Dk Nchimbi amesema amelibeba na wanakwenda kulifanyia kazi. Waziri wa Madani, Anthony Mavunde popote alipo atatue tatizo hilo.