Mpina aivaa wizara nzima ya Maliasili

Dodoma. Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kwa mara nyingine ameibua mjadala mkali bungeni safari hii akitoa kutoa wito kwa Bunge kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuchukua hatua kali dhidi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki pamoja na watendaji wote wa wizara hiyo.

Mpina, waziri wa zamani wa Mifugo na Uvuvi ambaye ambaye kwa siku za karibuni amegeuka mwiba kwa baadhi ya mawaziri, amesema waziri na watendaji hao wanapaswa kufukuzwa kazi kutokana na kushindwa kutatua kero za wananchi.

Alikuwa anazungumzia suala la unyanyasaji wa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi, alilosema linatekelezwa na maofisa uhifadhi waliopo chini ya wizara hiyo.

Mpina ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 3, 2024 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2024/25.

Amesema wananchi wanaoishi jirani na hifadhi wamekuwa wakikumbana na unyanyasaji wa mara kwa mara kutoka kwa wahifadhi, jambo ambalo linaathiri maisha yao ya kila siku.

Amesema jitihada za kuzungumza na viongozi wa wizara hiyo hazijazaa matunda yoyote, na hivyo ni muhimu kuchukua hatua kali ili kumaliza tatizo hilo.

Wito huo wa Mpina umepokelewa kwa hisia tofauti na wabunge wengine, baadhi wakiunga mkono na wengine wakitaka uchunguzi zaidi ufanyike kabla ya kuchukua hatua hizo kali.

Hata hivyo, hoja ya msingi iliyogusiwa na wengi ni kwamba, ni lazima kuwe na uwajibikaji wa moja kwa moja kutoka kwa viongozi wa juu wa wizara hiyo ili kuhakikisha haki za wananchi zinazingatiwa na kulindwa ipasavyo.

Mbunge huyo wa Kisesa amesema amesoma hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, lakini hajaona mahali popote ambako suala la mifugo kukamatwa limezungumziwa.

Amebainisha zaidi ya mifugo 11,438 imekamatwa na wafugaji wameshashinda kesi mahakamani, lakini haijarudishwa na hakuna kauli yoyote ya Serikali kuhusu suala hilo, jambo ambalo amesema ni kukiuka misingi na nguzo za utawala bora na utawala wa sheria.

Vilevile, Mpina amesema kumekuwa na ubambikiaji wa kesi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, ikiwemo kupigwa, kuteswa, kuuawa, na kunyang’anywa mifugo yao.

Amesema alishawahi kuwasilisha ushahidi wake ndani ya Bunge ambao ulikuwa sahihi na Waziri Mkuu Majaliwa alitoa maagizo 12 kuhusu kuzuia ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na sheria za nchi kwa baadhi ya watumishi wa hifadhi.

Vilevile, Mpina amesema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii nayo ilishwahi kusema na hata Mahakama imechoshwa na wahifadhi wanaonyanyasa wananchi.

Ametoa mfano wa hukumu ya rufaa na. 40809 ya mwaka 2023 iliyosomwa Aprili 24, 2024, na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Kamazima Kafanabo, ambapo mtuhumiwa Richard Changei Ng’ombe aliachiliwa huru na Jaji alitoa onyo kali.

“Sasa tangu kamati hiyo iliposema siku za nyuma, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi siku inaposoma tena maoni yake kuhusu makadirio ya wizara hii, hili si sawa,” amesema mbunge huyo.

Mbunge huyo amehoji juu ya kitendo cha wizara kukaa kimya na kupuuza maagizo ya Waziri Mkuu, Majaliwa.

Kutokana na mwenendo huo, Mpina ameliomba Bunge liiagize Serikali kupitia Waziri Mkuu iwafukuze kazi watumishi wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzia waziri hadi mfagiaji wa ofisi.

Pia, ameliomba Bunge liunde kamati ya kuchunguza mambo yanayoendelea kwa sababu (wabunge) hawawezi kuona wananchi wananyanyasika halafu wakae kimya.

Amesema ni lazima Bunge lichukue hatua ya kwenda kuchunguza hifadhi zote nchini.

Mei 31, 2024, akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa kamati ya Bunge inasimamia Maliasili na mazingira, Timotheo Mzava, alizungumzia suala hilo la unyanyaswaji wa wananchi.

Alisema uchambuzi wa kamati umebaini si tu malalamiko ya watu kubambikiwa kesi, bali kumekuwa na matukio ya wananchi kulalamikia kutaifishwa kwa mifugo yao kinyume na utaratibu.

Kamati hiyo iliitaka wizara kuhakikisha inafanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria, baadhi ya askari wanaokiuka maadili ya kazi yao na kutenda kinyume na sheria.

Pia, ilipendekeza kuboresha mtaala wa jeshi usu ili kuboresha utendaji wake.

Katika hatua nyingine, Mpina pia amezungumzia tukio la Desemba 27, 2023, ambapo mwindaji mkubwa duniani alijigamba kumkamata mamba mkubwa nchini Tanzania. Mwindaji huyo alionekana akimning’iniza mamba juu ya mti na kuanza kumchuna ngozi yake, jambo ambalo lilisababisha taharuki nchini.

Mpina ameeleza kushangaa kwa nini wizara hiyo halisemei jambo hilo.

“Hili suala lilienea kwenye mitandao ya kijamii lakini halijaonekana kwenye hotuba ya Waziri Kairuki. Mamba huyu mwenye urefu wa sentimita 495 (mita 4.98) alikuwa mrefu zaidi duniani, sasa kwa nini hakuwekwa katika hifadhi kwa ajili ya utalii, badala yake tukakubali awindwe na auawe?” amehoji.

Amesema Tanzania inatafuta vivutio vya utalii, “lakini tunaviua tulivyonavyo, kwa nini mamba huyu aliruhusiwa kuwindwa kwa utaratibu wa kawaida.”

Ameshauri hatua kali zichukuliwe na uchunguzi wa kina ufanyike juu ya suala hilo ili kubaini kama kuna ukweli juu ya utaratibu ulivyofanyika kuruhusu mamba huyo awindwe.

Hata hivyo, Januari 2 mwaka huu, Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa) ilisema Mwindaji wa Marekani, Josh Bowmer alimwinda mamba mkubwa mwenye urefu wa sentimita 493.8 katika kitalu cha Lake Rukwa GR kwa kibali halali na hakuna utaratibu uliokiukwa.

Katika mchango wake, Mbunge wa Mwibara, Charles Kajege, naye ameeleza kuwa kuna watu wanauawa na wengine kuachiwa ulemavu na askari wa wanyama pori kwenye maeneo mengi ya hifadhi, hivyo ameiomba Serikali kuja na suluhisho la kudumu.

Kuhusu kutokelezwa maagizo ya mahakaman, ametoa mfano wa Jaji Edward Mwensumo ambaye alikuwa na kesi dhidi ya wizara tangu mwaka 1998 ambayo alishinda lakini hadi sasa hajalipwa fidia.

Amesema haki iliyochelewa ni haki iliyonyimwa na amesisitiza kuwa Serikali inapaswa kumlipa haki yake kabla hajafa.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amemtaka Kajege kuwasilisha nakala ya hukumu hiyo ili hatua zichukuliwe.
 

Related Posts