Dar es Salaam. Tanzania imeibuka mshindi wa Tuzo ya Jumuiya ya Habari Duniani (WSIS 2024) nchini Uswisi.
Tuzo hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) Doreen Martin na kukabidhiwa kwa Rais wa Jumuiya ya Intaneti Tanzania Nazar Nicholas.
Utoaji wa tuzo hiyo umeshuhudiwa na Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye na ujumbe Tanzania alioambatana nao huko Uswisi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Ushindi huo umepatikana kupitia mradi wa Tanzania Digital Inclusion Project uliopo ndani ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) ulioshindanishwa na miradi mingine 90 kutoka nchi mbalimbali inayogusa eneo la upatikanaji wa habari na ujuzi.
Mradi wa Tanzania Digital Inclusion Project una miaka mitatu katika utekelezaji wake na unasimamiwa na Society Tanzania na unajihusisha na kuunganisha watumiaji wa intaneti ya kasi inayotumia mfumo wa ‘ushirikabando’ na mpaka sasa shule 10, ofisi ya Serikali ya mtaa moja, Ofisi ya Serikali ya kata moja, kituo cha polisi kimoja , Community Center moja na vikundi sita vya wajasiriamali vimeunganishwa.
Baada ya tuzo hiyo Nizar amesema mafanikio yote kidijitali yanayojitokeza nchini Tanzania ni kutokana na mchango mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameweka nguvu kubwa katika Wizara ya Habari Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuwezesha upatikanaji wa miundombinu ya intaneti.
Akielezea Nazar amesema intaneti ikitumiwa vizuri inaleta mafanikio lukuki huku akionesha mchango wa Intaneti katika maeneo mbalimbali yaliyofikiwa.
Ametoa mfano wa umuhimu wa intaneti katika kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na wanafunzi kupata maarifa yao kupitia intaneti.
Vilevile hata walimu wameoneka kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kutokana na kutumia muda mwingi kukaa shuleni kupakua maarifa ya kufundishia wanafunzi wao.
Nazar ameongeza kuwa hata shule zenye viwango vikubwa vya ufaulu, moja ya sababu za ufaulu wa shule hizo ni uwepo wa upatikanaji wa intaneti.
Amesema katika mradi wao wanaotekeleza wamefanikiwa kutoa mafunzo ya kidijiti kwa wananchi 1200, Walimu 197 na Wasichana 2000. Jambo ambalo linategemewa kuleta mabadiliko makubwa katika kutumia teknolojia ya kidijiti katika kuendesha shughuli mbalimbali za kisiasa kiuchumi na kimaendeleo.
Tanzania imekuwa ikishuhudia ongezeko la watumiaji wa huduma za intaneti na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dk Jabiri Bakari hivi karibuni inaonesha kwamba kuna watumiaji wa intaneti milioni 36.8 hadi Machi 2024 kutoka watumiaji milioni 35.9.