SHIRIKA la Protection International Africa (PIA), limeiongezea mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya Euro 122,440 (Sh. 34.5 milioni), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), kwa ajili ya ukuzaji nafasi ya kiraia na usawa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotoleo leo tarehe 3 Juni 2024, mkataba huo umesainiwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Mkataba huu wa mwaka mmoja unalenga kuendeleza mradi wa kukuza nafasi ya kiraia nchini kwa kuimarisha ushiriki wa makundi yote ya watetezi wa haki za binadamu. Shughuli zitakazotekelezwa kwenye mradi huu zinachangia moja kwa moja katika kutekeleza mpango mkakati mpya wa Mtandao (2023-2027),” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa, utekelezaji wa mkataba huo umeanza rasmi tarehe 1 Juni 2024 ambapo utafika tamati Disemba mwaka huu.
“Mojawapo ya wanufaika wa mradi huu ni watetezi wa haki za binadamu kutoka Bara ma visiwani Zanzibar. Pia, unatarajia kuongeza nguvu katika utetezi wa haki za binadamu nchini kea kuboresha mazingira yenye usawa kwa jamii nzima,” imesema taarifa hiyo.