RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema ana nia ya kujenga chuo cha masuala ya anga nchini Tanzania kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa shughuli ya Kutunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) katika sekta ya anga na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korea Aerospace University).
Amesema sekta ya anga ya Tanzania baina ya mwaka 2021 – 2023 imekua, kwani abiria wameongezeka kila mwaka kwa takriban asilimia 28 na pia idadi ya ndege zinazofanya safari za kimataifa zimeongezeka kutoka 26 hadi 33.
Idadi ya wasafiri wa ndani imeongezeka kwa asilimia 26.5 baada ya Covid-19 kutoka abiria milioni 3 hadi kufikia milioni 3.8 kwa mwaka wa 2023.
Rais Samia amesema nia ilikuwa kuwekeza kimkakati na hasa katika kufufua kampuni ya Air Tanzania Limited (ATCL) na kuendeleza miundombinu, ikiwemo mfumo wa kujenga rada na pia kukarabati na kupanua viwanja vya ndege kote nchini.
Kabla mwaka 2016, ATCL ilikuwa na ndege moja inayofanya kazi ambapo hadi kufikia Machi 2024 zimeongezeka ndege 14 za abiria na moja ya mizigo. Ndege 6 kati ya hizo zimenunuliwa katika kipindi cha miaka mitatu ikiwemo ndege ya mizigo.
Vile vile mtandao wake umepanuliwa kutoka maeneo 4 tu nchini hadi 24, ikiwemo safari katika miji minane barani Afrika na mitatu ya kimataifa (Guangzhou, Dubai na Mumbai).
Rais Samia amesema kufufua shirika hilo kumesaidia kuongeza mapato kutoka Shilingi za Kitanzania Bilioni 23 mwaka 2016/17 hadi 380.4 Bilioni mwaka 2022/23.
Pia soko la shirika la ATCL la safari za ndani limefika asilimia 53 asilimia kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23, huku idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka 2024.
Mbali na hapo, idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambalo ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023.
Rais Samia amesema kuwa mchango katika sekta ya anga kwenye Pato la Taifa la Tanzania umeongezeka kutoka asilimia 0.9 mwaka 2018 hadi asilimia 2.5 mwaka 2023.
Rais Samia anatarajia kesho kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu