Ramaphosa akubali anguko la ANC, awaachia wananchi

Johannesburg. Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo ni ushindi wa demokrasia.

 Katika matokeo hayo, African National Congress (ANC) imepata asilimia 40.18, ikifuatiwa na Democratic Alliance (DA) asilimia 21.81, uMkhoto we Sizwe (MK) asilimia 14.58, Economic Freedom Fighters (EFF) asilimia 9.52, huku vyama vingine vidogo vikikusanya jumla ya asilimia 13.91.

Matokeo rasmi yameonyesha ANC imeshinda viti 159 katika Bunge la Taifa lenye viti 400, ikishuka kutoka 230 hapo awali.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa ANC sasa lazima igawane madaraka, pengine na mpinzani mkuu wa kisiasa ili kuendelea kushikilia madaraka, jambo lisilo na kifani katika historia ya Afrika Kusini baada ya ubaguzi wa rangi.

Katika taarifa yake kwa wananchi, Rais Ramaphosa ametoa wito kwa vyama vya siasa vya Afrika Kusini kushirikiana kwa manufaa ya nchi.

“Waafrika Kusini wanatarajia vyama ambavyo wamevipigia kura kupata msingi wa pamoja, kushinda tofauti zao na kushirikiana kwa manufaa ya kila mtu,” Ramaphosa amesema baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya mwisho.

Akiwa na unyenyekevu kwa matokeo, ameita uchaguzi huo, “ushindi kwa demokrasia yetu.”

Vyama vya siasa sasa vina wiki mbili kupanga makubaliano kabla ya Bunge jipya kukaa kuchagua Rais, ambaye bado huenda akatoka ANC, kwa kuwa inabaki kuwa nguvu kubwa zaidi.

“Huu ni wakati kwa sisi sote kuweka Afrika Kusini kwanza,” Ramaphosa amesema.

Maofisa wa ANC mapema Jumapili walisema chama kilikuwa na unyenyekevu kwa matokeo hayo na hakuna cha kusherehekea,  lakini walimuunga mkono Ramaphosa aliyekuwa mpatanishi mkuu wa Mandela kumaliza ubaguzi wa rangi na walisema hawatakubali shinikizo la kumtaka ajiuzulu.

Matokeo mabaya yamechochea uvumi kwamba siku za Ramaphosa zinaweza kuwa zinahesabika  kutokana na matakwa ya mshirika wa muungano unaotarajiwa au kutokana na changamoto ya uongozi wa ndani.

“Hilo ni eneo lisiloruhusiwa,” Fikile Mbalula, katibu mkuu wa ANC, amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

“Je, tulifanya makosa? Ndio, tulifanya. Katika utawala na kwingineko,” amesema, akiongeza kuwa ANC sasa imejitolea kuunda Serikali  thabiti na inayoweza kutawala kwa ufanisi.”

Uongozi wa ANC utakutana Jumanne kupanga mambo yajayo katika chama hicho.

Cosatu,  kundi kubwa la vyama vya wafanyakazi Afrika Kusini na mshirika mkubwa wa ANC,  pia limeunga mkono Ramaphosa.

“Kitu muhimu ni kwamba muungano uongozwe na ANC na Rais Ramaphosa,” msemaji wa Cosatu Matthew Parks amesema.

Kabla ya uchaguzi wa Jumatano, ANC ilikuwa imeshinda kila uchaguzi wa kitaifa kwa wingi mkubwa tangu mwaka 1994, lakini katika muongo uliopita msaada wake umepungua.

Chama cha DA kilichoongozwa na Wazungu na kinachounga mkono biashara, kilipata asilimia 21.8 ya kura.

uMkhonto we Sizwe (MK), mkuki wa Taifa kwa lugha ya Zulu ni chama kipya kilichoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma kilichopewa jina baada ya tawi la zamani la kijeshi la ANC, kiliweza kuchukua asilimia 14.6, kikisababisha hasara kubwa kwa ANC.

Licha ya kufanya vizuri kuliko ilivyotarajiwa, MK imesema inazingatia kupinga matokeo hayo mahakamani.

Economic Freedom Fighters (EFF) ikiongozwa na kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC Julius Malema, wamepata asilimia 9.5.

Uwezekano wa ANC kuungana na EFF au MK umewafanya jamii ya wafanyabiashara wa Afrika Kusini na wawekezaji wa kimataifa kuwa na wasiwasi, ambao wangependelea muungano na DA.

Kiongozi wa DA, John Steenhuisen amesema kwenye kituo cha YouTube cha chama hicho kuwa walikuwa wameteua timu ya kuanza mazungumzo na vyama vingine kwa lengo la kuzuia muungano kama huo aliouita, “muungano wa siku ya mwisho.”

Chama kidogo cha Inkatha Freedom Party (IFP), cha kihafidhina cha Zulu chenye ngome katika Jimbo la KwaZulu-Natal kilichopata karibu asilimia 4 ya kura, kimekuwa na mkutano jana Jumapili kujadili hatua zake zijazo.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa, DA inaweza kuwa wazi kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na ANC, kuiunga mkono katika uamuzi muhimu kwa kubadilishana na kazi za juu bungeni.

IFP pia ingekuwa sehemu ya makubaliano kama hayo.

“Nafikiria (ANC) isingekwenda tu na DA. Labda wangekwenda na mtu kama IFP pia kwa sababu ya mtazamo kwamba DA ni chama chenye Wazungu wengi,” amesema Melanie Verwoerd, mchambuzi wa kisiasa.

Imeandikwa kwa msaada wa mashirika.

Related Posts