MSIMU wa 69 wa soka la Tanzania umekamilika kwa fainali ya Kombe la Shirikisho kufanyika visiwani Zanzibar na Yanga SC kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 6-5 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 0-0.
Yanga ambao pia ni mabingwa wa Ligi Kuu, wamefanikiwa kutetea mataji haya kwa msimu wa tatu mfululizo.
Walishinda mataji haya msimu wa 2021/22, 2022/23 na sasa 2023/24.
Sasa macho na masikio ya watu yanaelekezwa 2024/25. Lakini je, msimu wa 2023/24 ulikuwaje?
Ikiwa chini ya udhamini wa benki ya NBC na usimamizi wa Bodi ya Ligi, msimu wa Ligi Kuu wa 2023/24 ulikuwa bora sana yenye msisimko mkubwa kulinganisha na msimu uliopita wa 2022/23 na mingine mingi huko nyuma.
Ubora wa msimu huu umetokana na aina ya soka lililochezwa, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla, vilivyoleta ushindani katika maeneo mbalimbali ya msimamo.
I. NAFASI YA PILI ‘ILITRENDI’ KULIKO UBINGWA
Ni ukweli ulio wazi kwamba mbio za kuwania nafasi ya pili kati ya Azam FC na Simba zilileta msisimko kuelekea kumalizika kwa ligi kuliko mbio za ubingwa.
Raha ya mpira ni hali ya kutotabirika, lakini kuelekea kumalizika kwa msimu bingwa alishatabirika hivyo kupunguza msisimko.
Lakini mbio za nafasi ya pili zilikuwa na msisimko mkubwa kutokana na kutotabirika kwake.
Sare ya 1-1 ya Kagera Sugar na Simba pale Kaitaba, Mei 12, 2014, ndiyo kilele cha utamu wa vita vya nafasi ya pili.
Hii ilifanya Simba ambayo hadi hapo ilikuwa katika nafasi ya pili, kushuka hadi nafasi ya tatu kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku ikilingana alama na Azam FC ambayo ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC uliinua.
Hapo ndipo msisimko uliponoga na uliendelea kunoga hadi siku ya mwisho, Mei 28.
II. MBIO ZA UFUNGAJI BORA ZILIKUWA ‘FIRE’
Mbio za kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu zilikuwa bora na za kuvutia kuliko wakati wowote ule.
Sababu kuu ni aina ya wachezaji waliohusika. Feisal Salum wa Azam FC na Aziz Ki wa Yanga.
Kwanza hawa wote siyo washambuliaji halisi, ni viungo washambuliaji, hivyo kuleta mshangao kwa wafuatiliaji na kujiuliza wako wapi washambuliaji halisi?
Pili Feisal Salum ambaye alikuwa Yanga hapo kabla alikuwa akishindana na Aziz Ki wa Yanga, kitu ambacho kwa Yanga kilikuwa ‘tusi’ kubwa kwao endapo angeshinda vita hii.
Fei Toto ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga, amekuwa na msimu bora sana katika maisha yake na kutishia kutonesha ‘donda’ la wanayanga endapo angeshinda dhidi ya mchezaji wa Aziz Ki.
Lakini zaidi ya hivyo, ule ushindani wa muda mrefu wa kushushana pale juu uliongeza ladha kubwa sana.
Msimu uliopita mbio za ufungaji bora zilikuwa za upande mmoja kwa muda mrefu hadi mechi mbili kabla ya mwisho pale Saido Ntibazonkiza wa Simba alipofunga mabao matano dhidi ya Polisi Tanzania.
Mbio za msimu huu labda zinaweza kufanana na zile za msimu wa 2021/22 za George Mpole wa Geita Gold na Fiston Mayele wa Yanga.
Hata hivyo, ile hawa walikuwa washambuliaji halisi na pia hakukuwa na ile hisia ya kisasi kama ya msimu wa 2023/24 kwa mashabiki wa Yanga dhidi ya Feisal Salum.
III. NAFASI YA NNE NA KUSHUKA DARAJA
Coastal Union ya Tanga imerudi kwenye uga wa kimataifa baada ya miaka zaidi ya 30.
Mara ya mwisho kwao kushiriki mashindano ya kimataifa ilikuwa mwaka 1989 baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Muungano na kushirki Kombe la Washindi Afrika.
Mbio zao za kuwania nafasi hii zilitishiwa kwa kiasi fulani na KMC na TZ Prisons.
Hata hivyo, hadi raundi ya 25, timu yoyote chini ya tatu za juu ingeweza kushuka daraja.
MSIMAMO ‘TOP 3’ BAADA YA RAUNDI YA 25
P W D L F A PTS
1. Yanga 25 21 2 2 56 12 65
2. Azam FC 25 17 6 2 52 16 57
3. Simba SC 25 17 6 3 50 23 55
Ukitoa timu tatu za juu, timu yoyote kaunzia ya nne, kasoro Mtibwa Sugar pekee katika msimamo huo, ndiyo isingeweza kumaliza nafasi ya nne, lakini yoyote ingeweza kushuka
Hii nayo iliongeza ushindani hivyo kuleta ladha ya aina yake kuelekea mwisho wa msimu.
Japo msimu ulikuwa bora lakini bado kuna udhaifu wa kufanyia kazi.
Licha ya ubora wake lakini mabingwa wa msimu huu, Yanga SC, amefaidika zaidi na makosa ya waamuzi.
Nitatolea mfano mechi nne zilizoamua ubingwa.
Matokeo yakiwa 2-1, mchezaji wa TZ Prisons, Zabona Mayombya, alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na ilistahili kuwa penalti.
Lakini mwamuzi akamhukumu kwamba alifanya udanganyifu na kumpa kadi ya njano ambayo ilikuwa ya pili, hivyo kuzaa nyekundu.
Mechi ikaisha kwa ushindi wa Yanga wa 2-1 lakini baadaye ile kadi ikafutwa na Bodi ya Ligi kwa sababu haikuwa halali.
Maana yake mwamuzi aliwaonea TZ Prisons na kuwapa faida Yanga.
Matokeo yakiwa 0-0 na mchezo ukielekea mwishoni, Lameck Lawi wa Coastal Union anapewa kadi nyekundu ya moja kwa moja.
Coastal Union wanapungua na Yanga wanatumia kupungua huko na kupata bao la ushindi.
Baadaye kadi ikafutwa na Bodi ya Ligi kwamba ilitoka kimakosa…maana yake Yanga walifaidika na makosa ya mwamuzi.
Khalid Aucho alifanya madhambi ya shambulio la kudhuru mwili na alistahili kadi nyekundu ya moja kwa moja, lakini hakuonyeshwa.
Akaisadia timu yake kushinda katika mechi moja ya mechi zilizokuwa ngumu zaidi kwao.
Baadaye Aucho akafungiwa na Bodi ya Ligi kwamba madhambi aliyofanya hayakutakiwa kumuacha salama.
Kwa aliyeitazama mechi ile na kuona namna ilivyokuwa ngumu kwa Yanga, anaweza kukubaliana nami hapa kwamba endapo Aucho angeonyeshwa kadi nyekundu, hali ingekuwa tofauti.
Aubrey Chirwa wa Kagera Sugar alifunga bao zuri katika mchezo huu lakini mwamuzi akalikataa kimakosa.
Baadaye mwamuzi huyo akafungiwa lakini tayari Yanga walishafaidika, na matokeo yanabaki yale yale.
Ukiangalia msimamo wa ligi wa mwisho wa msimu na ukijaribu kuondoa hizi alama ambazo zilipatikana kimakosa, utaona kabisa Yanga wamekuwa mabingwa kwa kufaidika na makosa ya waamuzi, licha ya ubora wao.
Tatizo la viwanja limeendelea kuwa sugu kwenye mpira wetu.
Tena kufungwa kwa Uwanja wa Mkapa na Uhuru kumeongeza changamoto kwa Dar es Salaam.
Lakini hata viwanja vingine vinavyotumika bado vina hali mbaya sana.
Rais wa TFF, Wallace Karia, amesikika akisema msimu ujao wataongeza vigezo vya uwanja wa kutumika kwa Ligi Kuu.
Hili ni jambo la heri kwa sababu vigezo vya sasa viko chini sana. Viwanja vinavyopasishwa kutumika kwa Ligi Kuu vina ubora wa chini sana.
Licha ya ukweli kwamba ligi yetu imepiga hatua kubwa sana kwa ubora na mafanikio ya ndani na nje ya uwanja, lakini bado inatiwa doa kubwa sana na imani za kishirikina.
Kila siku ya mechi lazima kuwepo na matukio kadhaa yanayoashiria ushirikina.
Na hii ni kuanzia mashabiki hadi wachezaji…hatari sana.
Mamlaka zimekuwa zikichukua hatua za kinidhamu kila mara lakini bado tatizo linaongezeka.
Hii inaonyesha kwamba jamii yetu kama taifa ina tatizo kubwa sana kuamini ushirikina.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu na makamu wa pili wa Rais wa TFF, Steven Mguto, amenukuliwa akisema msimu ujao timu itakayobainika kufanya matukio yanayoashiria ushirikina, itapokwa alama.
Labda hii inaweza kusaidia kutibu hili tatizo, ingawa pia inaweza kuzua utata zaidi kama mashabiki wa timu A wataamua kuingia uwanjani kwa hila na kujidai ni wa timu B kwa kuvaa hata sare za upande mwingine (za timu B) kisha kufanya vitendo vinavyoashiria ushirikina ili wapinzani wao hao (timu B) wapokwe alama. Umakini utahitajika hapa, sababu unaweza kuzaa tatizo jingine la timu kuhujumiana ili kuhakikisha wapinzani wanakatwa pointi.
Lakini yote juu ya yote, msimu wa 2023/24 ulikuwa bomba sana…sasa tuusibiri msimu wa 2024/25!