Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema wagonjwa 36,404 kutoka mikoa 14 wamefikiwa katika huduma za matibabu kutoka kwa madaktari bingwa na bobezi, wanaozunguka wilaya mbalimbali nchini.
Kambi hiyo iliyozinduliwa rasmi Mei 6 2024 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu imewafikia wagonjwa hao kwa kipindi cha siku 25 hadi kufikia Mei 31 2024 na kumekuwa mahitaji makubwa ya wananchi kutaka kuwaona watalaamu hao.
Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 3, 2024 na mwakilishi wa wizara hiyo, Notigera Ngaponda wakati shughuli ya kuwakabidhisha madaktari bingwa na bobezi 30 watakaoendesha kambi ya matibabu katika vituo na hospitali sita za Mkoa wa Dar es Salaam.
“Katika watu 36,404 baadhi wamegundulika kuwa na changamoto ya magonjwa mchanganyiko yakiwamo ya ndani, uzazi, watoto, usingizi na upasuaji. Kambi au kampeni hii, imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi,”amesema Ngaponda.
Amesema miongoni mwa hospitali watakazokwenda madaktari bingwa hao ni Kivule, Mbagala, Kigamboni, Mnazi Mmoja na Mabwepande.
Amefafanua kuwa kila hospitali au kituo cha afya kitakuwa na watalaamu watano waliobobea katika maeneo mbalimbali wakiwamo madaktari wa usingizi na ganzi, upasuaji na wale wa kina mama na watoto.
Ngaponda amesema lengo la kambi hizo ni kuwasogezea huduma wananchi hasa wasiokuwa na uwezo wa kuwafikia madaktari bingwa na bobezi.
Amesema hiyo ni awamu ya nne ya kampeni itakayoitimishwa Juni 28.
“Utakuta mwananchi ana tatizo lakini hana uwezo wa kuzifikia huduma za kibobezi, sasa Serikali imeamua kuwasogezea. Hawa wabobezi wanapotoa huduma inawarahisishia na kuwapunguzia makali ya gharama za kuzipata huduma,”amesema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohamed Mang’una ameishukuru Serikali kupeleka wataalamu hao watakaoanza kutoa huduma kuanzia Juni 3 hadi Juni 7 katika maeneo watakayopangiwa.
“Ujio wao utaleta fursa kwa madaktari watakaowakuta kwa ajili ya kubadilisha uzoefu na mawazo, naishukuru Serikali kuja na wazo hilo linalolenga kuwahudumia Watanzania wengi zaidi,” amesema.
“Mkoa wa Dar es Salaam tumejipanga vizuri kutoa huduma hizi, niwaombe wananchi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya afya na hospitali ambazo watalaamu hawa watakuwa wakitoa huduma,”amesema Dk Mang’una.
Mmoja wa madaktari bingwa, Dk David Mazengo kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, amesema kumekuwa na mwitikio kwa wananchi kujitokeza kupata matibabu katika kambi hizo.
“Kuna magonjwa mengi hayawezekani kutibika katika kituo cha afya au hospitali, lakini ujio wetu sisi tumewezesha wananchi kupata matibabu papo hapo,”amesema Dk Mazengo.