Auawa akidaiwa kujaribu kuwatoroka Polisi

Songea.  Francis Ngonyani, mkazi wa Songea, mkoani Ruvuma amefariki dunia baada ya kupigwa risasi mguuni na Polisi akidaiwa kujaribu kuwatoroka.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne Juni 4, 2024 eneo la Lizabon, Songea mjini.

Ngonyani anatuhumiwa kuwa kinara wa kuvunja maduka ya wafanyabiashara wa Songea mjini na kuiba vitu mbalimbali, vikiwamo vifaa vya ujenzi, pembejeo za kilimo na spea za magari.

Akizungumza na wandishi wa habari leo ofisini kwake mjini Songea, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya amesema Ngonyani anayedaiwa kuvunja madauka 15 ya wafanyabiashara, amefariki dunia baada ya kupigwa risasi akijaribu kuwakimbia Polisi.

Amesema Polisi waliweka mtego na  kufanikiwa kumkamata mhalifu mmoja akiwa na vifaa vya kukatia mabati na kuvunjia milango – mkasi, tindo, nyundo na bisibisi.

“Baada ya kumkamata mtuhumiwa ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa, alimtaja Ngonyani kuwa ndiye anayeshirikiana naye kufanya uhalifu huo na akataja na mahali alipojificha kwenye nyumba moja iliyopo Mtaa wa Lizabon,” ameeleza kamanda huyo.

Amesema baada ya taarifa hiyo, Polisi walienda kwenye nyumba hiyo, wakaizingira na kumtaka mtuhumiwa atoke ajisalimishe, lakini aligoma akajificha juu ya dali, kitendo kilichosababisha askari afyatue risasi juu ya kumuamuru ashuke, naye alishuka na kujisalimisha.

“Lakini wakati akipanda kwenye gari la Polisi alishtuka kumuona mtuhumiwa mwenzake kwenye gari hilo, akahamaki na akawaponyoka askari na kuanza kukimbia.

“Ndipo askari walifyatua risasi juu huku wakimkimbiza na kumtaka asimame ajisalimishe lakini hakutii amri, ndipo wakampiga risasi moja mguuni akaanguka,” amesimulia kamanda huyo.

Kamanda Chilya amesema mtuhumiwa aliwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Songea kwa matibabu lakini kwa kuwa alikuwa amevuja damu nyingi, alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu.

Chilya amedai taarifa zinaonyesha Ngonyani aliingia Songea Aprili 4, mwaka huu akitokea Dodoma alikokimbia baada ya mshirika mwenzie wa uvunjaji, aliyetambuliwa kwa jina la Japhet Nyoni kuuawa.

“Tumeambiwa huyu (Nyoni) ndiye alimfundisha  Ngonyani namna ya kukata nyaya za kamera, kuficha uso na kuvunja, naye ameuawa baada ya kufanya matukio ya uhalifu,” amesema Chilya.

Wakai huohuo, Kamanda huyo wa Polisi amesema wataendelea kumshikilia mtuhumiwa wa awali mpaka wamalize upelelezi, kisha watamfikisha mahakamani.

Wakizungumza na Mwananchi kuhusu mtu huyo aliyeuawa, Ramadhan Hyera mkazi wa Manispaa ya Songea amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo akisema linafanikiwa kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vinashika kasi.

Naye Agnetha Ndimbo, mfanyabiashara wa duka la bidhaa mbalimbali mjini Songea, amesema matukio ya uvunjaji wa maduka yameibua hofu kwao na kwa wananchi kwa ujumla.

“Matukio haya yanatokea sana siku hizi, ni bora Polisi walivyoamua kufanya msako, labda kutapoa,” amesema Ndimbo.

Related Posts