Bares atoa masharti manne Mashujaa

BAADA ya kufanikiwa kubaki salama Ligi Kuu, Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdalah Mohamed ’Bares’ amesema ripoti aliyowasilisha kwa uongozi iwapo itafanyiwa kazi ipasavyo, msimu ujao timu hiyo itashangaza wengi.

Mashujaa ambayo ilishiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu, licha ya kupitia misukosuko ya matokeo yasiyoridhisha, ilifanikiwa kubaki salama ikiwa nafasi ya tisa kwa pointi 34.

Bares aliliambia Mwanaspoti kuwa ripoti yake kwa menejimenti anahitaji usajili wa wachezaji saba, akiwamo straika kuziba nafasi ya Adam Adam aliyetimka.

Alisema mengine ni kuingia kambini mapema na kuwabakiza wachezaji waliong’ara kwa ajili ya msimu ujao, lakini kuendeleza ushirikiano ndani na nje ya uwanja ili timu hiyo ifanye vizuri zaidi.

“Msimu ujao tutakuwa na mabadiliko, presha za kushuka daraja hatutaki tena zijitokeze, nimekabidhi ripoti ikiwa na mapendekezo manne ikiwamo usajili bora, kubaki na nyota waliofanya vizuri, lakini hitaji la wachezaji saba akiwamo straika,” alisema Bares.

Kuhusu hatma yake kikosini humo, alisema ni mapema sana kulizungumza kwani bado hajamaliza mkataba wake kwa tarehe aliyosaini, lakini matarajio yake ni kubaki na timu hiyo iwapo uongozi utamhitaji.

Alikiri wazi kuwa ligi haikuwa nyepesi, huku akieleza kuwa kilichowapa wakati mgumu ilikuwa usajili ambao haukuzingatia mahitaji lakini hata muda wa maandalizi haukutosha.

“Bado nina siku kadhaa mkataba uishe, hivyo naamini tunaweza kuzungumza ili nibaki hapa, lakini hatutakiwi tena kukurupuka kusajili, ndio maana nimewasilisha mapema ripoti ili tujipange,” alisema kocha huyo.

Related Posts