Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekopa Sh813.6 bilioni kwa mikopo sita ya miradi ya maendeleo na dhamana za Serikali kwa taasisi 14 zenye thamani ya Sh185.73 bilioni tangu mwaka 2020.
Hadi kufikia Machi 2024, deni la Taifa linalodhaminiwa na SMZ limefikia Sh1.105 trilioni kati ya fedha hizo deni la Serikali ni Sh919.36 bilioni na dhamana ya deni kwa taasisi ni Sh185.73 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 609.3 ikilinganishwa na deni lililorekodiwa mwaka 2020 la Sh155.8 bilioni.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma alipojibu swali katika Baraza la Wawakilishi Chukwani, Unguja.
Swali hilo la msingi liliulizwa na Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman akitaka kujua mikopo mingapi imekopwa na yenye thamani kiasi gani na mikakati ya Serikali kulipa deni hilo.
“Hadi sasa deni hili linaendelea kulipwa na Serikali kwa wakati. Mikakati iliyopangwa na Serikali katika kulipa mikopo ni pamoja na mikopo inayochukuliwa inakuwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo nchini ambayo matokeo yake yatachangia katika ukuaji wa pato la Taifa,” amesema.
Mkakati mwingine wa kurejesha mikopo hiyo, amesema ni kuendelea na juhudi za kuongeza wigo wa kukusanya mapato ambayo sehemu yake hutumika katika kulipia mikopo hiyo.
Pia, kuhakikisha deni linalipwa kwa wakati.
Amesema Serikali imekuwa na mpango maalumu wa ulipaji wa madeni hayo sambamba na kuwa na hesabu maalumu ambayo hutumika kulipa madeni pale yanapoiva.