Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko amekerwa na watendaji wa vitengo vya mazingira kwenye wizara na taasisi kudhani kuwa hawana shughuli za kufanya na wakati mwingine kutotengewa bajeti.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 3, 2024 wakati akifungua maadhimisho ya Wiki ya Mazingira, Dk Biteko amesema kazi utunzaji wa mazingira imeachiwa na wizara moja tu ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
“Wewe (Waziri Dk Selemani Jafo) kazi yako ni kusimamia sera na kila wizara ina kitengo cha mazingira, ni bahati mbaya kuna wakati vitengo hivi kwenye wizara na taasisi vimewekwa watu ambao wanadhani hawana shughuli za kufanya, havitengewi bajeti,”amesema.
Amesema pia hakuna shughuli inayofanywa na wizara na taasisi hizo badala yake kazi hiyo wameachiwa wizara moja tu ya Muungano na Mazingira.
“Inafika mahali ukitaka kuzungumzia mazingira basi utakuta wizara moja tu, wakati kila wizara ina kitengo cha mazingira na wajibu wake ni kuhakikisha suala la mazingira linashughulikiwa,” amesema.
Dk Biteko ameagiza kupatiwa taarifa ya idara za mazingira za wizara na taasisi ambazo hazijashiriki maadhimisho hayo ili zijulikane kwa lengo la kupewa ushauri zaidi.
Amesema hayo kwenye maadhimisho hayo inawezekana vitengo vya baadhi ya wizara na taasisi havikwenda kwa kudhani kuwa wana mambo makubwa kuliko mazingira.
“Niwaambie ndugu zangu mliopo serikalini mazingira ni kila kitu,” amesema.
Dk Biteko amesema baadhi ya vitengo havifanyi kazi na havitengewi bajeti lakini ni lazima vifanye kazi zake ipasavyo kwa kuwa kila shughuli ina athari kwenye mazingira.
“Nitoe wito kwa watendaji wote wa wizara na taasisi ambao kitengo chake cha mazingira hakijaja hapa, ni muhimu tujue ni kitengo gani cha wizara gani hakikuleta mtu ili tupate namna ya kuwashauri vizuri, haina maana tukija hapa tukasema, tukapiga picha na tukaondoka,” amesema.
Amesema kazi ya kutunza mazingira haipaswi kusemewa na mtu mmoja, bali kusemwa na watu wote serikalini na kwa uzito ulele kwenye wizara, ofisi za wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.
Aidha, Dk Biteko ametoa rai kwa Watanzania kuendelea kutumia teknolojia bunifu ambazo ni sehemu ya suluhisho ya changamoto ya uchaguzi wa mazingira na kujipatia kipato kwa kuingia kwenye biashara ya hewa ukaa (kaboni),
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Selemani Jafo amesema maadhimisho hayo yametumika kufanya shughuli mbalimbali zilizolenga katika utunzaji wa mazingira.
Amesema pia watatumia maadhimisho hayo kuzindua sera ya uchumi wa buluu na utoaji wa tuzo na hamasa ya biashara ya hewa ukaa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema wilaya zote za Mkoa wa Dodoma zimeazimia kutenga maeneo matatu kwa ajili ya biashara ya hewa ukaa.
Amesema hadi sasa Wilaya ya Mpwapwa imeonesha kuwa na sifa ya kufanya biashara hiyo na kuwa mchakato unaendelea kwa wilaya zingine.