Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ikikabidhi Bandari ya Dar es Salaam kwa Kampuni ya DP World, Serikali inaangalia namna ya kufanya upanuzi wa bandari hiyo ili kuendana na ongezeko la mizigo inayohudumiwa.
Hiyo ni baada ya baadhi ya wamiliki wa migodi kutoka nchi jirani pia kuonyesha nia ya kuanza kutumia Bandari ya Dar es Salaam na Kigoma kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema DP World ilianza kazi Aprili 7 mwaka huu licha ya kuwa TPA inamalizia baadhi ya vitu kabla ya kuachia kila kitu chini ya mwendeshaji huyo.
Hayo yameelezwa leo Juni 3, 2024 wakati Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Ali Possy alipofika Bandari ya Dar es Salaam kuangalia namna shughuli mbalimbali zinazofanyika baada ya Dp World kuanza utekelezaji akiambatana na ujumbe kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).
Oktoba 22, mwaka jana Serikali iliingia makubaliano na DP World kupitia mikataba mitatu iliyosainiwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika bandari hiyo kwa miaka 30.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mrisho amesema kilichobakia chini ya TPA ni baadhi ya meli ambazo zilikuwa zimesajiliwa katika mifumo ya TPA lazima wazihudumie.
“Shughuli hazijasimama pamoja na makabidhiano hayo, changamoto kama wadau fulani walizungumza kuhusu mifumo ndiyo hiyo tunayosema transition tunaimarika sana na hiyo mifumo wanayoizungumzia ya DP World, nadhani baada ya muda tutakaa sawa zaidi, kazi zinaendelea, gati zote zimejaa meli na meli zinahudumiwa,” amesema Mrisho.
Amesema DP World tayari inafanya kazi maeneo yote isipokuwa kuhudumiwa meli zilizokuwa zimeingizwa katika mifumo ya TPA.
“Sasa hivi ninachozungumza kila kitu sasa kinasomeka kwa DP World,” amesema Mrisho.
Amesema kwa ufanisi unaoonekana, uhudumiaji wa mizigo utaongezeka mara mbili.
“Hadi Aprili mwaka huu tayari tulikuwa tumehudumia tani 19.6 milioni ikilinganishwa na lengo tulilokuwa tumepewa katika mwaka huu wa fedha la kuhudumia tani zaidi ya milioni 22,” amesema Mrisho.
Katika kuonyesha namna ufanisi utakavyopatikana, Mrisho amesema tayari DP World imefunga mitambo mbalimbali itakayowawezesha kuhudumia mizigo bandarini hapo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dk Ali Possi amesema wakati watoa huduma hao wakianza kazi lengo la Serikali ni kuona ufanisi unakua kama ilivyokua imetarajiwa.
Amesema tayari wapo wamiliki wa migodi kutoka nchi jirani ambao wameonyesha nia ya kutumia Bandari ya Dar es Salaam na ile ya Kigoma jambo ambalo ni fursa, hivyo Serikali inaangalia uwezekano wa kuongeza eneo la bandari ili kuendana na ukuaji huo.
“Tunatarajia kupata gati si chini ya tano kama tukifanikiwa kuongeza zilizo na urefu wa mita 300, tukiongeza gati shughuli zetu za bandari zitaimarika na biashara itaongezeka sambamba na mapato ya kikodi,” amesema Dk Possi.
Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi chini ya Shirika la uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Nashoni Sigara amesema huenda ikachukua muda kwa wafanyakazi wa ndani na watumiaji wa bandari kuelewa mifumo hiyo na na namna wanavyopaswa kuitumia.
“Ni vyema wakawekeza nguvu na muda katika kuwawezesha watumiaji na wafanyakazi kuelewa mifumo na taratibu walizokuja nazo bandarini hapo,” amesema Sigara.