Serikali yatoa kauli malalamiko ya kodi, matumizi ya EFD

Dodoma. Wakati Serikali ikiwataka wananchi kuwasilisha malalamiko ya kodi kupitia namba ya bure, imeeleza changamoto inazopitia katika ukusanyaji kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki za EFD.

Pia Kamati ya Bunge ya Bajeti imezungumzia tatizo la malalamiko ya kodi, ikibainisha masharti ya kumlinda mteja kwenye Sheria ya Sekta ndogo ya Fedha ndiyo suluhisho la mikopo ‘kausha damu.’

Hayo yameelezwa leo Jumanne Juni 4, 2024 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya mpango na bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/25.

Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh18.17 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25. Mwaka 2023/24, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh15.87 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.

Dk Mwigulu amesema Bodi ya Rufani za Kodi imeanzisha mfumo wa kupokea malalamiko kwa njia ya simu ambao mlalamikaji au mtoa taarifa anaweza kuyawasilisha kwa kupiga simu ya bure namba 0800111022.

“Jitihada hizo zimewezesha ongezeko la mwamko wa wananchi na walipakodi,” amesema.

Amesema hadi Aprili 2024, Bodi ya Rufani za Kodi imepokea mashauri ya kodi 437 ya kodi bishaniwa ya Sh3.5 bilioni na imesikiliza na kutoa uamuzi wa mashauri 388 ya kodi bishaniwa ya 2.7 bilioni na Dola za Marekani 439,281.

“Baraza la Rufani za Kodi limesajili mashauri 112 ya kodi bishaniwa ya Shilingi bilioni 2,790 (Sh2.79 trilioni), mashauri 64 ya kodi bishaniwa ya Sh137.9 bilioni yamesikilizwa na kutolewa maamuzi na mashauri 56 ya kodi bishaniwa ya Shilingi bilioni 2,510 (Sh2.5 trilioni yako katika hatua mbalimbali za usikilizaji na kutolewa maamuzi,” amesema.

Amesema Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imepokea malalamiko 40, imesuluhisha malalamiko 22 na malalamiko 18 yapo katika hatua mbalimbali za usuluhishi.

Kwa upande wake, Kamati ya Bunge ya Bajeti katika maoni yaliyosomwa na Makamu Mwenyekiti, Twaha Mpembenwe imezungumzia malalamiko hayo ikisema Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB), bado kuna changamoto kwa kuwa wajumbe wake hawako sehemu zote za nchi.

“Katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, TRAB ina wajumbe katika mikoa 14. Kamati ilibaini mikoa 12 (Manyara, Katavi, Kigoma, Kilimanjaro, Iringa, Lindi, Mara, Mbeya, Njombe, Rukwa, Songwe na Tabora haina wajumbe,” amesema.

Kukosekana wajumbe katika Bodi, amesema kunasababisha mashauri ya kodi kuchukua muda mrefu kusikilizwa na kuwa na mlundikano wa mashauri ambayo hayajasikilizwa.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2022/23 imeainisha mashauri 967 ya kodi kwenye Bodi ya Rufani za Kodi zenye thamani ya Sh10.48 trilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh5.65 trilioni sawa na asilimia 117 ikilinganishwa na Sh4.83 trilioni za mwaka wa fedha 2021/22. Ongezeko hilo lilichangiwa na kuchelewa kwa uteuzi wa wajumbe muhimu wa kusikiliza kesi,” amesema Mpembenwe.

Amesema kamati ilijulishwa kuwa taratibu za uteuzi wa wajumbe katika mikoa hiyo zinaendelea.

“Kwa msingi huo, kamati inaishauri Serikali kukamilisha taratibu za uteuzi katika mikoa 12 iliyobaki, ili kuharakisha usikilizwaji wa kesi za kodi katika maeneo hayo. Sambamba na hilo, kamati inaishauri Serikali kuweka utaratibu utakaowezesha mjumbe kutoka mkoa mmoja kusikiliza kesi katika mkoa mwingine, ili kupunguza mlundikano wa kesi,” amesema.

Kuhusu changamoto za utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2023/24, Dk Mwigulu amesema wizara imekabiliana na huduma hafifu ya matengenezo ya mashine za EFD.

“Kukosekana kwa mtandao na mwamko mdogo wa wananchi kudai na kutoa risiti za kielektroniki za EFD; kuongezeka kwa mahitaji ya ziada ya rasilimali fedha kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na baadhi ya walipakodi kuficha taarifa za miamala ya kibiashara na kuendelea kuwepo kwa biashara za magendo, hususan mipakani na mwambao wa bahari,” amesema.

Dk Mwigulu amesema ili kukabiliana na changamoto zilizojitokeza, wizara imechukua hatua kadhaa kama vile kuhamasisha matumizi ya mfumo wa VFD kutoa risiti kama mbadala wa mashine za EFD.

Amesema wizara itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kudai na kutoa risiti za kielektroniki, kuboresha mifumo ya usimamizi wa mapato, ikiwemo doria mipakani na mwambao wa bahari ili kudhibiti biashara za magendo na udanganyifu.

Dk Mwigulu ametaja vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kutafuta na kukusanya mapato ya Sh44.19 trilioni kati ya maoteo ya Sh49.35 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali.

Related Posts