HATIMAYE sasa Simba imeanza ule umafia wake, baada ya kuingilia dili la Yanga na sasa ipo mwishoni kumalizana na kiungo wa Singida Fountaine Gate, Yusuph Kagoma.
Awali gazeti hili liliripoti mpango wa Yanga kuwinda saini ya kiungo huyo kwa lengo la kuwa msaidizi wa Khalid Aucho kwenye timu hiyo itakayocheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Kagoma kimeliambia Mwanaspoti kuwa staa huyo muda wowote kuanzia sasa atakuwa mali ya Simba kutokana na mazungumzo ya pande zote mbili kwenda vizuri.
“Suala la Yanga kumfuata Kagoma halina kificho, ni kweli walifanya hivyo lakini mazungumzo hayakwenda vizuri kama ilivyo kwa upande wa Simba ambayo ina 95% kumpata na kuwa mchezaji wao msimu ujao,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Haikuwa rahisi kama unavyofahamu mafahari wawili hao Simba na Yanga wakikutana sehemu moja kila timu ilionyesha nia lakini Wekundu wa Msimbazi walikuwa na nia zaidi kwani hawakukata tamaa licha ya vikwazo vingi hadi walipofikia muafaka,”kilisema chanzo hicho.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Mwanaspoti zinabainisha kuwa Simba tayari wamempa ofa kiungo huyo kusaini mkataba wa miaka miwili kwa thamani kubwa zaidi ya ofa waliyotuma watani zao Yanga ili kumng’oa staa huyo ambaye bado alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Singida Fountaine Gate.
Alipotafutwa Rais wa Singida Fountaine Gate, Japhet Makau alisema muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi na wao wametoa baraka zote kwa mchezaji endapo ofa yao itakamilika.
“Kagoma alikuwa nje ya timu kwa muda kwa ruhusa maalumu na kuhusiana na mpango wa kuondoka ndani ya timu kwetu tumetoa baraka zote,” Alisema.
Endapo kiungo huyo mambo yataenda kama walivyopanga ataenda kuungana na Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute ambao wote wanacheza kiungo mkabaji na muda mwingine Ngoma na Kanoute wamekuwa wakitumika kama viungo washambuliaji.
Kiungo huyo ambaye amejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kinachojiandaa na mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Zambia alikuwa na kiwango cha juu msimu uliopita wa ligi.