Dar es Salaam.Ni ukweli usiopingika kwamba takribani kila kaya nchini Tanzania ina kijana aliyehitimu shahada ama stashahada, lakini hana ajira wala shughuli ya kumuingizia kipato.
Ikumbukwe kuwa elimu ni uwekezaji ambao ni sawa na biashara nyingine na kila mzazi humpeleka mtoto wake shule kwa malengo ya kupata maarifa na kipato.
Lakini sasa hali ni tofauti. Vijana waliohitimu kwa mbwembwe bado wanasalia nyumbani kuomba vocha kwa wazazi.
Katikati ya malalamiko ya ukosefu wa ajira nchini anaibuka msomi gwiji wa fani ya fani ya jiolojia duniani, Profesa Sospeter Muhongo na kukonga nyoyo za wengi kuhusu mbinu za kukabili donda ndugu la ajira.
Profesa huyo nguli, ambaye ana machapisho zaidi ya 150 katika fani yake, alisikika kwenye vyombo vya habari akisema ajira zipo nyingi duniani, ilimradi tu vijana watambue na kujikita kwenye fani zinazouzika sokoni.
Kwa mujibu wa msomi huyo nguli, vijana wanapaswa kusomea fani za kuwa wazalishaji wa programu (software developer), wanasayansi wa takwimu (data scientist), wachambuzi wa usalama wa taarifa (information security analysts), wauguzi wabobezi, wachambuzi wa usimamizi (management analysts) pamoja na kuhakikisha wana utaalamu wa akili bandia.
Alisema ajira hizi tayari zina soko kubwa nchini India na nchi nyingine nyingi duniani zenye uchumi wa daraja la kwanza.
Tanzania ina kila sababu ya kutopuuza mawazo yake. Tunapaswa kuyafanyia kazi kwa kuwekeza kwenye fursa hizo tajwa hasa kipindi hiki tunavyopigia chapuo mabadiliko ya mitalaa na tahasusi mpya.
Mtaalamu wa sayansi ya kumpyuta na mbobezi wa uzalishaji wa programu, Alome Gabagambi anasema kwa uzoefu alioupata nchini India, nchi hiyo inaamini katika kubadili mitalaa kulingana na hitaji la soko, huku akibainisha kuwa si ajabu mhitimu aliyekaa nyumbani kwa miaka mitatu kuomba ajira na akajikuta ujuzi aliosomea umeshapitwa na wakati.
Gabagambi anayefanya kazi Dubai, anasema ni lazima vijana wa Kitanzania wachukie hali ya kubweteka na kutafuta maarifa duniani kila uchao, huku akibainisha kuwa kuna ajira ambazo mtaalamu anatafutwa badala ya yeye kutafuta kazi.
“Kuna wakati unaweza kuitiwa kazi sehemu tano hadi 10 ukaanza kuchagua kulingana na dau wanalokutajia. Kazi zipo nyingi kwenye masuala ya teknolojia tatizo ni uwezo wa walio wengi kukidhi vigezo. Elimu yetu inapaswa kujikita kujenga ujuzi wa mtu binafsi pasipo kuwekeza kwenye nadharia,” anasema.
Moja kati ya mambo yanayotofautisha nchi tajiri na zile masikini ni ajira. Katika nchi mfano zile za Ulaya, watu ni wachache na ajira ni nyingi.
Lakini katika mataifa masikini, hasa barani Afrika, watu ni wengi na kazi ama ajira ni chache. Afrika ndilo bara lenye vijana wengi kuliko bara lolote.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, asilimia 70 ya wakazi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wako chini ya umri wa miaka 30.
Nchi zinapokuwa na vijana wengi, maana yake wengi wao hutaka kufanya kazi ili kujenga maisha yao. Neema ya Afrika kuwa na vijana wengi imekuja na gharama ya ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana hao.
Kuna namna mbili ya kuangalia ukubwa wa tatizo la uhaba wa ajira. Mosi, kuangalia matukio yanayoashiria moja kwa moja uwepo wa tatizo hilo. Pili, kuziangalia takwimu kwa mujibu wa Serikali au mashirika yanayoshughulika na tafiti za aina hiyo.
Juni 2014, zaidi ya watu 1000 walijitokeza katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kufanya usaili wa maombi ya kazi katika Idara ya Uhamiaji. Tovuti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, ilieleza kulikuwa na nafasi 70 pekee zilizohitaji waajiriwa wapya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umasikini Tanzania (REPOA) ya 2019, takribani vijana milioni moja wanahitimu kila mwaka kutoka taasisi mbalimbali za kielimu, huku idadi ya ajira zinazozalishwa kutoka serikalini na sekta binafsi ni 250,000, kwa wastani wa kila mhitimu anatumia miaka 5.5 kupata ajira.
Pamoja na Serikali kuwashinikiza vijana kutokimbilia ajira serikalini na badala yake waweke mkazo katika kujiajiri, bado nachelea kusema kwamba haingii akilini mhitimu wa shahada ya uhandisi ama ualimu ajiajiri kwenye kibanda cha M-Pesa ama kuuza mgahawani na bado hiyo tuiite ajira.
Ajira ni sharti iendane na uwekezaji alioufanya mtu kwenye fani stahiki. Siamini kama vijana wetu wanakaa chuo kikuu kwa miaka zaidi ya minne kujifunza kutengeneza simu kwenye vibanda vidogo vutuo vya mabasi mitaa ya Mawasiliano na Kariakoo jijini Dar-esa Salaam!
Katika mizunguko yangu kwa takribani mwezi mmoja mitaa ya Sinza, Mawasiliano na Kariakoo Mtaa wa Kongo, nilihakikishiwa kuwa wafanyabiashara ndogondogo ni vijana waliohitimu shahada katika fani mbalimbali ila wameamua kujikita kwenye shughuli nyingine mbadala.Nchi nyingi duniani zimekuwa zikikutana na changamoto hii, hususani katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia anguko la uchumi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita vinavyoshudiwa mashariki mwa bara la Ulaya kati ya Urusi na Ukraine.Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO, 2022), takribani vijana milioni 73 sawa na asilimia 23.3 ya vijana duniani kote hawana ajira.
Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani, imekuwa ikishuhudia changamoto ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana wanaohitimu vyuo vikuu na vyuo vya kati. Hali hiyo imeanza kushuhudiwa kuanzia miaka ya 2010 hadi sasa baada ya msukumo kuwa umewekwa kwenye mpango wa elimu ya msingi na sekondari kwa wote bila malipo.