Spika Tulia aagiza kamati iwaite, kuwahoji wakurugenzi NSSF, PSSSF

Dodoma. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameielekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi wa Jamii kuwaita na kuwahoji wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi za jamii nchini kuhusu madai ya wanufaika kutakiwa kulipa fedha za michango ambazo waajiri wao hawakuilipa mifuko hiyo, ili wapatiwe mafao yao.

Dk Tulia ametoa agizo hilo jana bungeni jijini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu kutokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko.

Ameomba mwongozo huo kutokana na swali la Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge aliyehoji changamoto ya baadhi ya waajiri kutolipa michango ya watumishi wao na kusababisha mifuko ya hifadhi kuwataka wahusika wenyewe kuchangia kuziba mapengo.

Katika swali la nyongeza, Kasinge amesema kumekuwa na changamoto ya waajiri kutopeleka michango ya watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

“Walimu ambao baadhi yao wamelipwa waliambiwa wakachangie wenyewe katika mifuko hii badala ya waajiri ili waweze kulipwa,” amesema.

Amesema mstaafu aitwaye Hadija Bungurumo ni miongoni mwa ambao walilipwa mafao ya kustaafu baada ya kuambiwa akachangie mwenyewe.

Amehoji Serikali kama huo ndiyo utaratibu unaotakiwa kufanyika.

Baada ya swali hilo, Dk Tulia ameuliza Serikali iwapo mawaziri wanaoshughulika na mafao wapo bungeni, akajibiwa hawapo.

Majibu hayo yalimfanya Dk Tulia kumweleza mbunge kuwa swali lake linahitaji majibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na siyo Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Baada ya muda mchache, alisimama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera na Uratibu), Jenista Mhagama ambaye amesema wamepokea jambo hilo jipya na wanaomba walichukue ili wizara inayohusika ilitolee ufafanuzi.

Hata hivyo, Mhagama amesema mafao yote yanalipwa kwa kuzingatia sheria. Na kwa mujibu wa sheria hakuna mahali mstaafu anatakiwa kulipia michango yake mwenyewe ili apate mafao.

Dk Tulia amesema kitendo cha mstaafu kuambiwa achangie ili alipwe mafao yake ni kizito na kikubwa.

Amesema suala la madai ya mafao ya kustaafu la walimu hao ni la muda mrefu na kumtaka Mhagama kufuatilia ili waweze kupewa mafao yao.

Dk Tulia amemuhoji Kasinge wastaafu hao hawajalipwa tangu mwaka gani na kujibiwa ni tangu mwaka 2018.

Kasinge amesema wapo wastaafu wa mwaka 2020, baadhi walipeleka michango yao na kulipwa.

Baada ya majibu hayo, Dk Tulia amemtaka mbunge huyo kupeleka majina kwa Serikali ili waendelee kufuatilia kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, baada ya kipindi cha maswali na majibu Matiko ameomba mwongozo wa spika kuhusu suala hilo.

Amesema changamoto ya malimbikizo ya madeni ya michango halipo kwa walimu tu bali na kada nyingine.

Matiko ameomba mwongozo wa Spika wa nini kifanyike kuhusu suala hilo ambalo Serikali imekuwa ikisema ni jambo jipya wakati limeshawahi kuelezwa.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza, Mhagama amesema utaratibu wa wastaafu kuambiwa kupeleka michango ili walipwe mafao yao haukubaliki.

Mhagama amesema ndiyo maana wakati akizungumza lilipoulizwa swali, aliomba  Serikali kupewa ushirikiano ili wizara inayoshughulika na pensheni ipate nafasi ya kushughulikia jambo hilo kwa umakini na ukamilifu.

“Umetupa maelekezo tumepokea na tunaendelea kulishughulikia. Siyo kwamba Serikali matatizo haya imekuwa haiyashughulikii bali imekuwa ikiendelea kuyashughulikia. Lakini tuko tayari kushughulikia kila linapojitokeza na kuendelea kutoa maonyo kwa watumishi wa Serikali wanaowalazimisha kulipa fedha wakati ni kinyume cha utaratibu,” amesema.

Akihitimisha mjadala huo, Dk Tulia amesema aliwahi kuelekeza Serikali kuleta marekebisho ya sheria ili mifuko ya hifadhi inayochelewesha mafao ilipe riba kwa mstaafu kama wanavyotoza riba kwa waajiri wanaochelewesha michango ya wanachama.

Amesema jambo hilo linaendelea kufanyiwa kazi na Serikali na kwa sababu wanasubiri hilo lifanyike siyo rahisi kulitolea mwongozo.

“Nalipeleka suala hilo kamati inayohusika waweze kulifuatilia kwa ukamilifu. Serikali itapeleka majibu kule na kama iko sababu ya kuwaita wakurugenzi hawa waitwe huko ili wakaeleze kule kwenye kamati ni mazingira gani mwajiriwa anatakiwa kulipa fedha za madeni ya michango,” amesema.

Amesema huko ndiko watakapopata majibu hata yanayohusiana na ucheleweshaji wa mafao kwa wastaafu.

Spika amesema kamati hiyo watawashauri nini wafanye na kuhusu jambo hilo watalitoa kwa Bunge wakati wa uwasilishaji wa taarifa za kamati.

Related Posts