Tanga. Zaidi ya taa 600 za barabarani katika Jiji la Tanga zimebainika kuwa hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Wafanyabiashara na watumiaji wa maeneo hayo wamelalamika kuathiriwa na hali hiyo waliyodai kuwa husababisha ajali na wananchi kuporwa mali zao.
Wafanyabiashara wa maeneo ya barabara ya 12, 15 na 21 na mitaa mingine wakizungumza na Mwananchi Digital jana usiku Juni 2, 2024, wamesema changamoto hiyo ni ya muda mrefu.
Mfanyabiashara wa eneo la Barabara ya 21, Yasini Omari, amesema eneo hilo lina taa zaidi ya sita ambazo hazifanyi kazi, hivyo wanategemea mwanga kutoka maduka makubwa ya jirani.
Amesema giza linawaathiri kwa sababu biashara zao hazionekani vizuri.
“Taa hizi zilipokuwa zinawaka, hata biashara tulikuwa tunafaya vizuri, lakini sasa hivi wateja nao wanahofia usalama na kuibiwa ikifika saa 12:30 jioni, wengi hawaji kufanya manunuzi kwa sababu hiyo,” amesema Omari.
Aisha Hoseni, mama lishe katika Barabara ya 15, amesema eneo hilo lina taa ambazo pia haziwaki. Wanategemea mwanga wa kutoka vibaraza vya watu na lolote likitokea kama umeme umekatika ni changamoto kwao.
Kaimu Mhandisi wa Jiji la Tanga, Jumanne Jumaaa, alipoulizwa na Mwananchi juu ya hilo, amekiri kuwepo kwa changamoto ya taa hizo kutowaka na kwamba baadhi ya nyaya zimeibiwa ndiyo maana taa hizo haziwaki.
“Watu wanahujumu hii miundombinu, hata tukizirudishia nyaya hizo wanaziiba na taa hizo zinatumia umeme wa kawaida,” amesema Jumaa.
Hata hivyo, amesema hivi sasa wanapanga mkakati wa kuzifufua upya taa hizo.
Alipoulizwa kwanini hawafungi taa zinazotumia umeme wa jua amesema; “tatizo ni betri zake ambazo zimekufa, lakini utaratibu wa kuzibadilisha upo kwa maeneo yote ambayo zimeonekana kutokuwaka.”
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, akiwa kwenye ziara ya kukagua taa hizo hivi karibuni, alisema wamebaini zaidi ya taa 600 za jiji hilo hazifanyi kazi usiku.
Batilda alisema taa hizo ni zile zilizofungwa katikati ya jiji na maeneo maarufu mkoani humo. Alitoa wiki moja kwa uongozi wa jiji na mamlaka nyingine zinazohusika kuhakikisha taa hizo zinafanya kazi kama inavyotakiwa kwani inawezekana.
“Tumekuta taa 600 ambazo zimeunganishwa kwenye umeme wa Tanesco haziwaki na wameamua kutokulipa. Ndani ya wiki hii taa hizi za Tanesco ziwake, zile zenye changamoto za waya zikaguliwe wakati wakiendelea kusubiria zile nyingine za sola ambazo wameziagiza,” alisema Balozi Burian.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Sebastiana Ndanda, amesema tayari wameagiza taa nyingine zaidi ya 100 kwa ajili ya kufungwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ili kurudisha huduma kama awali na wananchi wapate mwanga usiku.
Jiji la Tanga linakusanya mapato ya zaidi ya Sh21 bilioni ambapo asilimia 60 ya fedha hizo inatakiwa kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo kukarabati miundombinu.