Wakati mchezo wa play off hatua ya kwanza kwa timu za Tabora United na JKT Tanzania ukipigwa leo Jumanne, presha imeonekana kutawala ndani na nje ya uwanja katika vita ya kubaki Ligi Kuu.
Timu hizo zinatarajia kukutana mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabo-ra, huku Tabora United wakiwa ndio wenyeji wa mechi hiyo.
Wapinzani hao wamekutana katika mchujo huo baada ya kumaliza nafasi ya 13 na 14, huku Mtibwa Sugar na Geita Gold zikiwa zimeshuka daraja moja kwa moja na kuzipisha Ken Gold na Pamba Jiji zilizopanda.
Tabora United ndio ulikuwa msimu wao wa kwanza kucheza Ligi Kuu, sawa na JKT Tanzania ambao walipanda kwa pamoja, japokuwa Maafande hao waliwahi kushiriki misimu miwili nyuma kabla ya kushuka daraja.
Kila timu inahitaji ushindi ili kujiweka mazingira mazuri kabla ya kukutana kwenye mchezo wa marudi-ano Juni 8, ili kujua hatma ya nani kukutana na Biashara United ya Championship inayosubiri mpinzani na nani kubaki kwenye ligi.
Katika mechi hizo mshindi wa jumla atabaki Ligi Kuu, huku mwingine akicheza na Biashara United ili-yofanikiwa kuweka matumaini ya kupanda Ligi Kuu baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeya Kwanza.
Biashara United ilimaliza Championship nafasi ya nne, huku Mbeya Kwanza ikimaliza nafasi ya tatu, ambapo walipokutana kwenye dakika 180, timu hiyo ya mkoani Mara ilishinda nje ndani.