VIDEO: Serikali yakana kuipa bahari, madini Korea Kusini

Dar es Salaam. Serikali imefafanua juu ya mkopo wa Sh6.7 trilioni uliosainiwa kati yake na Korea Kusini, ikieleza kuwa haijatoa sehemu ya bahari wala madini ya kimkakati.

Ufafanuzi huo umetolewa leo Juni 4, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kuwapo kwa taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii, zikionyesha namna Korea itakavyokwenda kunufaika na rasilimali za Tanzania baada ya kutoa mkopo huo.

Kupitia mtandao, Sauti ya Amerika (VOA), Juni 3, mwaka huu ilichapishwa habari iliyoeleza kuwa kupitia mikopo iliyotolewa kwa Tanzania na nchi ya Ethiopia, Korea Kusini sasa itapata fursa ya kuchimba madini muhimu katika nchi za Afrika.

Chombo hicho pia kilieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amesaini mkataba utakaoiruhusu Korea Kusini kutumia bahari yake na madini yanayotumika katika teknolojia ya nishati safi kama Nickel, Lithium na Graphite.

Taarifa hii ilibua mvutano katika mitandao ya kijamii hususan ule wa X, jambo ambalo lilianza kuwaibua viongozi mbalimbali kuja kujibu hoja kabla ya Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo, Mobhare Matinyi kusimama mbele ya waandishi wa bahari kutoa ufafanuzi.


Serikali yakana kuipa bahari, madini Korea Kusini

Matinyi amesema mkopo wa zaidi ya Sh6.7 trilioni ambao umetolewa kwa Serikali ya Tanzania ni ule wa riba nafuu ambao utaanza kulipwa baada ya miaka 25 kupita na malipo yake yatachukua miaka 40.

 “Serikali haijaweka rehani kitu chochote au mali yoyote kama inavyoelezwa katika mijadala inayoendelea na mkopo huo hauna masharti yoyote ya kuweka rehani kitu chochote,” amesema Matinyi.

Mkopo huo umetolewa kwa ajili ya miradi ya miundombinu chini ya mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya uchumi wa Jamhuri ya Korea (EDCF).

Kusainiwa kwa mkopo huo ni moja ya matukio ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliyashuhudia katika ziara yake inayoendelea nchini Korea Kusini, ambapo pia hati mbili za maelewano zilisainiwa ikiwemo itakayohusisha ushirikiano katika sekta ya uchumi wa buluu na ile inayohusu madini ya kimkakati.

“Katika uchumi wa buluu kunatarajiwa kuwa na ushirikiano katika utafiti, shughuli za uvuvi na kutoa mafunzo kwa watu wa ndani kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa buluu,” amesema Matinyi.

Katika makubaliano ya uendelezaji wa madini ya kimkakati, Matinyi amesema yanalenga kuifanya Tanzania kuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya madini yake sambamba na kufanya utafiti kujua madini hayo yanapopatikana.

“Kwa wastani nchi yetu imeshafanyiwa utafiti, kwa hakika asilimia 16 ya nchi yetu ndiyo imefanyiwa utafuti ili kujua madini hayo wapi yanapatikana, tunataka kushirikiana na korea kujua madini hayo wapi yanapatikana,” amesema Matinyi.

Mbali na Matinyi, viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura wametoa ufafanuzi juu ya suala hilo katika mtandao wa kijamii wa X.

“Tanzania inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu,” ameandika Togolani.

Kwa upande wake, Waziri wa Uwekezaji na Mipango, Profesa Kitila Mkumbo alijibu hoja hiyo kwa kusema kuwa makubaliano yanayohusu madini ya kimkakati yanalenga kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika utafiti, uchimbaji na kuongeza thamani ndani ya nchi.

Related Posts