Wanafunzi 5,818 kujiunga kidato cha tano Zanzibar

Unguja. Wanafunzi 5,818 wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano kisiwani hapa.

Idadi hiyo ya wanafunzi imeongezeka kutoka 4,415 mwaka 2023 hadi kufikia 5,818 mwaka 2024 sawa na asilimia 21. Kati ya hao wasichana ni 3,352 na wavulana ni 2,466.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Juni 4, 2024, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Abdugulam Hussein amesema kati ya wanafunzi hao, waliotoka shule binafsi na kutimiza sifa za kujiunga kidato cha tano ni 1,070.

“Idadi kamili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka 2024 ni 5,818, ambapo wa shule za Serikali ni 4,645 na kutoka shule binafsi ni 1,070 na watahiniwa wa kujitegemea ni 103,” alisema Naibu Waziri Abdugulam.

Amesema wanafunzi hao wamegawanywa katika tahasusi za masomo ya sayansi wakiwa 3,485, sanaa 1,955, uchumi na biashara 200, kompyuta 63 na wanafunzi watakaoendelea na masomo yao katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST) kwa masomo ya ufundi ni 115.

Kutokana na idadi ya wanafunzi kuongezeka, amesema wizara imeongeza shule sita, ili asiwepo mwanafunzi atakayekosa nafasi.

Majina ya wanafunzi hao amesema yanapatikana kupitia tovuti ya wizara (website ya WEMA) www.moez.go.tz

Amesema wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano wanatakiwa kuripoti shuleni Julai mosi, 2024 kuanza masomo na kwamba maelezo zaidi kuhusu kanuni na sheria za shule zitatolewa na na uongozi wa shule.

Kwa wanaotakiwa kuripoti Chuo cha Sayansi cha Karume, amesema watatakiwa kuripoti Oktoba, 2024 na maelekezo zaidi watapata wakifika chuoni.

Baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa akiwemo Rashid Issa Issa, amesema amefurahi kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na kuahidi kusoma kwa bidi, ili kutimiza ndoto zake za kuwa rubani baadaye.

Related Posts