Wananchi waitwa kutoa maoni Dira ya Maendeleo 2050

Dar es Salaam. Tume ya Mipango, imewaita wananchi kushiriki kutoa maoni ikiwamo kutuma ujumbe mfupi kuhusu dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.

Dira ya Taifa ya maendeleo ni picha au maono kuhusu mustakabali tarajiwa wa maendeleo ya nchi katika siku za usoni.

Wito huo umetolewa leo Jumanne Juni 4, 2024 Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Rais-Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru alipokuwa akizungumza na wanahabari kuhusu kongamano la maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Mafuru amesema kongamano hilo, litafanyika Juni 8,2024 kuanzia saa tatu asubuhi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na  Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

“Tunatamani wananchi wote washiriki katika mchakato huu ili kujibu maswali yafuatayo; je, dira 2050 inamtaka Mtanzania wa aina gani? Je, tunataka jamii ya aina gani ya Kitanzania ifikapo 2050? Je, tunataka nchi ya aina gani ifikapo 2050?

 “Tume ya Mipango inawahimiza wananchi wote kutoa maoni yao na kuchangia katika mjadala mzima kuhusu dira 2050,”amesema Mafuru.

Mafuru amefafanua kuwa ushiriki unaweza kuwa katika namna nyingi, ikiwamo majukwaa ya umma, tafiti, mijadala ya mitandao ya kijamii na mikutano ya kijamii.

 “Maoni ya kila Mtanzania ni ya thamani katika kuandaa dira ya mwaka 2050 itakayokidhi matarajio na mahitaji ya Taifa,” amesema Mafuru.

Kwa mujibu wa Mafuru, tume hiyo ina jukumu kubwa la kutoa elimu kuhusu Tanzania inayotakiwa ifikapo 2050, ili kuwaandaa vema wananchi wote kutoa maoni yao yatakayochangia kwa asilimia 100 katika kuiandaa dira ya Taifa 2050.

Amesema Tume ya Mipango itafanya kazi kwa karibu na waandishi wa habari, wadau wa maendeleo na wananchi mmojammoja ili kuhakikisha kila Mtanzania anafahamishwa, anashiriki na anachangia kikamilifu katika kuunda mustakabali wa Taifa.

 “Dira ya Taifa inapaswa kutupa picha ya matarajio ya nchi kufikia uchumi wa juu wa kati ifikapo mwaka 2050, hivyo Tume ya Mipango inasisitiza uelewa na hamasa kwa umma ili kila mtu kushiriki kutoa maoni yake,”amesema.

Julai 5, 2023 katika hafla ya kuapishwa kwa watendaji wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alimweleza Mafuru kuwa ana kazi tatu, ambazo ni kubainisha hali halisi ya maendeleo ya nchi, kubadilisha mwelekeo wa nchi kimkakati na kuongoza maandalizi ya dira ya Taifa ya mwaka 2050.

Related Posts