Watu sita mbaroni wakituhumiwa kukutwa na meno ya tembo 12

Mwanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro  linawashikilia watu sita akiwamo raia mmoja wa Kenya kwa tuhuma za kukutwa na vipande 12 vya meno ya tembo.

Akizungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa hao leo Jumatatu Juni 3, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema watuhumiwa wanne walikamatwa Mei 30, 2024 na vipande sita vya meno ya tembo vikiwa ndani ya mifuko miwili ya salfeti eneo la Kata ya Kivisini huku wengine wawili wakikamatwa na vipande vingine sita vikiwa ndani ya begi dogo la kusafiria eneo la Kata ya Kileo, wilayani humo.

“Katika operesheni ya ukamataji wa makosa mbalimbali iliyofanyika kuanzia  Mei 20 hadi Juni 2, 2024 tumefanikiwa kukamata vipande 12 vya meno ya tembo na watuhumiwa sita ambao wote ni wanaume,”amesema Kamanda Maigwa.

Amesema Mei 30, mwaka huu, saa 2:00 usiku katika Kitongoji cha Kitoghoto, Kata ya Kivisini, wilayani Moshi, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana  na askari wa Hifadhi ya Taifa (Tanapa) walifanikiwa  kuwakamata watu wanne akiwamo raia wa nchi jirani ya Kenya wakiwa na mifuko miwili ya salfeti ndani ikiwa na mbegu za alizeti na katikati kukiwa na vipande sita vya meno ya tembo.

“Katika tukio jingine Juni mosi, 2024 majira ya saa 4:00 usiku huko maeneo ya Kata ya

Kileo, Wilaya ya Mwanga tulifanikiwa

kuwakamata watu wawili wakiwa na begi

ndani yake kukiwa na meno ya tembo vipande sita,” amesema Kamanda Maigwa.

Amesema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya utaratibu wa kiupelelezi kukamilika.

“Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayejihusisha na uangamizaji wa nyara za Serikali bila kujali wadhifa wake,” amesema kamanda huyo.

Related Posts