Yanga yabeba mabilioni baada ya kutwaa Ligi Kuu, FA

FEDHA ndefu! Hivyo ndiyo unaweza kusema baada ya Yanga kufanikiwa kutwaa ubingwa wa FA ambao unawafanya wakusanye kitita kikubwa cha fedha msimu huu baada ya awali kuchukua kombe la Ligi Kuu Bara.

Yanga msimu huu, imeweka rekodi nzito ikikusanya jumla ya Sh6.5 bilioni kutoka kwa wadhamini, zilizotokana na makombe mawili iliyochukua huku ikifika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hiki ni kiwango kikubwa cha fedha kwa timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuwahi kuzoa baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi na Kombe la FA, tofauti na misimu kadhaa iliyopita.

Taji la kwanza la ubingwa msimu huu, Yanga imechukua Kombe la Ligi Kuu Bara ambalo linawafanya Yanga wasubiri kuiona 100 milioni ikiingia kwenye akaunti yake.

Yanga imetwaa ubingwa huu baada ya kukusanya pointi 80 kwenye michezo 30, huku Azam ikishika nafasi ya pili na Simba nafasi ya tatu.

Ndani ya ubingwa huo wa ligi Yanga kwa kumaliza nafasi ya kwanza kwenye ligi, imechukua Sh500 milioni kutoka kwa wadhamini wa haki za matangazo kwa televisheni, ikifuatiwa na Azam watakaochota Sh300 milioni wakati Simba iliyomaliza nafasi ya tatu ikivuna Sh 250 milioni na Coastal nafasi ya nne 200.

Baki hapo hapo kwenye ligi, ubingwa huo ukaipa tena kiasi cha Sh 150 milioni kutoka kwa wadhamini wao wakuu, kampuni ya SportPesa kwenye mkataba wao, makubaliano ya Yanga na kampuni hiyo ni kwamba kama itatwaa ubingwa itapewa bonasi ya kiasi hicho cha fedha.

Ubingwa Shirikisho Sh112m

Hatua ya kulichukua taji hilo kama ambavyo Yanga ilifanya juzi mbele ya Azam FC inaifanya ivune tena kiasi cha Sh 112 milioni kutoka kwa wadhamini wao hao wakuu wa SportPesa, iliposhinda kwa penalti 5-6.

Ubingwa Shirikisho Sh200m

Ubingwa huo wa shirikisho ambao Yanga iliutwaa juzi kwa kuichapa Azam FC kwa penalti 6-5 inawafanya wadhamini wa michuano hiyo kuipa timu hiyo kitita cha shilingi milioni 200.

Yanga pia iliingia mkataba binafsi wa maudhui na matangazo ya televisheni na Azam Media ambao kwa hatua ya kuchukua ubingwa tu inajihakikishia kiasi cha Sh 1.1B kupitia mafanikio hayo.

Achana ba fedha hizo za ndani, Yanga pia msimu huu ilivunja rekodi yake ikiishia hatua ya robp fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikibakiza hatua ndogo tu kutinga nusu fainali ilipotolewa kwa matuta na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Hatua hiyo ikawapa Yanga kiasi cha Sh 2.3 bilioni kwa kuishia hatua hiyo kiasi ambacho hapa nchini Simba pia ilikivuna ilipoishia baada ya kung’olewa na bingwa wa mara ya pili mfululizo Al Ahly ya Misri.

Mapato hayo, yanaifanya Yanga kuvuna jumla ya kiasi cha Sh6.5 Bilioni kutoka kwa wadhamini hao mbalimbali ambapo hakuna timu inayoweza kuwafikia kwa mkwanja huo.

Simba wao msimu huu imejihakikishia kiasi cha sh 2.8 Bilioni kwa hatua ambayo imefikia ikivuna fedha nyingi kutoka kwa CAF baada ya timu hiyo kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa ikichukua kiasi cha sh 2.3 Bilioni.

Wekundu hao pia wamevuna 250 milioni kwa kushika nafasi ya tatu kwenye ligi, fedha ambazo zinatolewa kutoka Azam Media kupitia mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni kwenye ligi.

Simba imevuna pia kiasi cha Sh50 milioni kwa kuchukua ubingwa wa Muungano huku wadhamini wao Mbet wakiwapa jumla ya Sh150 milioni kwa kutinga hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa Sh50 milioni wakati ilipotinga robo fainali ikawapa tena Sh100 milioni na kuwafanya wekundu hao kuvuna jumla ya Sh2.8 bilioni.

Related Posts