Dar es Salaam. Katika kuleta uendelevu na kuwa na mwenendo mzuri wa utunzaji wa mazingira, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), kimewajengea uwezo wanafunzi kidato cha pili wa shule ya sekondari ya wasichana ya Jangwani jijini Dar es Salaam.
Mafunzo yaliendeshwa na klabu ya mazingira ya wanafunzi ya AKU yakiambatana na upandaji wa miti katika shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mazingira duniani inayosheherekewa kila Juni 5 ya kila mwaka.
Akizungumza leo Jumatano Juni 5, 2024 kwa niaba ya klabu ya mazingira ya wanafunzi wa AKU, Adelphina Kimario amesema wamekwenda Jangwani kwa lengo la kuadhimisha siku ya mazingira duniani kwa kuwapa mafunzo na uelewa wanafunzi wa shule kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
“Tunataka tuwahamasishe watunze mazingira wakiwa wadogo, maana ukiwapata wanafunzi utakuwa umefikisha ujumbe katika kundi kubwa la watu kwa haraka zaidi ndio maana tumekuja hapa kujumuika na wenzetu,” amesema Kimario.
“Tumewajengea uwezo kuhusu elimu ya mazingira kwa nadharia na vitendo ambapo tumepanda miti pamoja ambayo wataitunza na kuhakikisha inastawi vizuri,” amesema Kimario.
Naye, mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo, Isfahan Bugenyi amekishukuru chuo hicho kwa jitihada zake, akisema kinaonyesha namna kilivyokuwa na ushirikiano na kuthamini mazingira.
“Mafunzo tuliyoyapata yanatuongezea ujuzi na upendezeheshaji wa shule yetu katika suala nzima la utunzaji wa mazingira.Elimu tuliyoipata leo itatusaidia katika suala nzima la uhifadhi wa mazingira,” amesema Bugenyi.
Mwalimu wa shule hiyo, George Mapunjo amesema AKU wamekuwa wadau wao wakubwa wakishirikiana katika nyanja mbalimbali za kielimu na mazingira na sio mara ya kwanza chuo kwenda shuleni hapo.
“Ni muhimu kukumbushana kama jamii kwamba mazingira ndio kitu cha kipekee kinachotusaidia binadamu. Siku ya mazingira lazima itekelezwe kwa vitendo ikiwemo kupanda miti kama ambavyo leo tumepanda na wenzetu wa AKU,” amesema Mapunjo.