Bibi  wa miaka 77 auawa kwa kukatwa shingo

Moshi. Mkazi wa Kijiji cha Nakombila, Kata ya Kimochi, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Jenny Mtesha (77) ameuawa kwa kukatwa shingo kwa mundu na mtu anayedaiwa kuwa ni mjukuu wake (Jina tunalihifadhi) aliyetaka kumpora bibi huyo  Sh 240, 000.

Inadaiwa kuwa, tukio hilo lilitokea Juni 3, 2024  baada ya  bibi huyo kutoka sokoni, kisha mtuhumiwa  akitaka amsindikize kwenda kuokota kuni za kupikia chai ya jioni.

Alipotafutwa  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuzungumzia madai hayo simu yake ilipokewa na msaidizi wake aliyesema kamanda yupo kwenye kikao cha Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi.

“Samahani kamanda yupo kwenye kikao cha Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi naomba umpigie baadaye,” alisema msaidizi huyo.

Hata hivyo, alipotafutwa baadaye simu yake iliita bila kipokewa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Wilfred Sekei  amedai kuwa  mtuhumiwa huyo alimwambia Jenny waende kuokota kuni za kupikia chai ya jioni.

“Bibi akakubali kwenda naye kumbe alikuwa amebeba mundu (panga la kukatia majani), wakiwa wanatembea akiwa nyuma alimkata shingo kwa nyuma,” amedai mwenyekiti huyo.

Sekei amedai kuwa baada ya kijana huyo kudaiwa kutekeleza mauaji hayo alichukua Sh240,000 zilizokuwa ndani ya mfuko wa nguo alizovaa Jenny na kwenda kuzificha.

“Huyu kijana aliona afanye hivyo kwa sababu huyu bibi anapenda kutembea na fedha zake tena ana mfuko wake ndani ya nguo anaopenda kuficha fedha zake na aliona njia rahisi ya kuzipata ni lazima amuue,” amedai Sekei.

Amedai kuwa baada ya kukamatwa na kupekuliwa na polisi walimkuta na Sh245,000.

Elika Mtesha ambaye ni  mke mwenzake Jenny amedai kuwa mauaji hayo yamewaumiza wana familia.

“Kama alikuwa na shida na hela si angeomba tu badala ya kuua. Mimi niko mbali kidogo na familia, nilipigiwa simu kwamba mke mwenzangu ameuawa, nilienda eneo la tukio nikakuta yule mama kweli amekufa,” amedai Elika.

Hata hivyo, amedai kuwa aliwatafuta polisi waliofika eneo la tukio na kumkamata kijana huyo akiwa eneo alilofanyia mauaji.

“Polisi walipofika waliukuta mwili bado uko chini, wakamsaka huyu kijana ambaye mwanzo inasemekana alikimbia lakini baadaye akarudi nyumbani ndipo wakamkamata,” amedai Elika.

Related Posts