Caf yaanza na Coastal Union, Azam

Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limezitaka timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kukamilisha usajili wake mapema.

Caf juzi ilitoa taarifa ya kuonyesha kalenda ya michuano ya kimataifa, Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, huku ikionekana kuwa timu zina siku chache tu kuanzia sasa kukamilisha usajili wake.

Yanga na Azam zitashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku timu za Simba na Coastal Union zikishiriki Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu ya ratiba iliyotolewa na shirikisho hilo ambayo inaonyesha mchakato wa kuanzia mwanzo wa mashindano hayo hadi siku ya fainali ya msimu wa 2024/2025, inaonyesha kuwa hatua ya awali mechi zake zitaanza Agosti  16 na 18, huku hatua ya makundi ikitarajiwa kupigwa Oktoba hadi Desemba 2024.

 Ratiba hiyo inaonyesha kuwa fainali italazimika kuwa Mei mwaka 2025 mfumo ukiwa uleule wa nyumbani na ugenini.

Hii ina maana kuwa timu za Azam na Coastal Union ambazo zinaonekana kuwa zitaanzia hatua ya awali zinatakiwa kuhakikisha zimekamilisha usajili wake hadi Julai 20, huku zile za Simba na Yanga ambazo zitacheza hatua ya kwanza zikipewa kutoka  Julai 21 hadi Agosti 31 kuwa siku ya mwisho ya kuwasilisha usajili wake Caf.

Hii ina maana kuwa timu za Azam na Coastal zinatakiwa kuanza mchakamchaka wa usajili sasa kama zinataka kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

Kwa usajili wa Tanzania dirisha lake linatarajiwa kufunguliwa Juni 15 ambalo litakwenda hadi Agosti 31, mwaka huu.

Hata hivyo, shirikisho hilo limeendelea kuweka mkazo kuwa hakuna timu ambayo itatolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikashuka Shirikisho ukiwa ni mfumo kama ambavyo ulikuwa msimu uliopita.

Kwa upande wa usajili katikati ya mashindano inaonekana kuwa umeonekana kuwa timu ambazo zitafanikiwa kuingia hatua ya makundi zitapewa nafasi ya kusajili wachezaji wapya saba huku usajili huo ukifunguliwa Januari  Mosi na kufungwa Januari 31, 2025.

“Utaratibu huu wa usajili umefanyika ili kuhakikisha kila timu inapata nafasi ya kushiriki kwa usawa kwenye hatua zote za mashindano haya,” ilisema taarifa ya shirikisho hilo.

Akizungumzia ratiba hiyo Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Azam FC, Zacharia Thabit, amesema wao wapo tayari na walishakamilisha usajili wao kabla hata ligi haijamalizika.

“Sisi tupo tayari hata kama Caf watasema tuwape majina leo, tulishamaliza usajili wetu na kila mmoja ameona aina ya wachezaji ambao tumewatangaza.

“Hatuna presha, kila kitu tumekiweka sawa na nikuhakikishie tu malengo yetu msimu huu ni kufika nusu fainali ya michuano hii, ndiyo maana mmeona jinsi ambayo tumejipanga vyema,” alisema Zacharia maarufu kama Zaka Zakazi.

Katibu Mkuu wa Coastal Union  Omar Ayoub, ameweka wazi kuwa wanaendelea na mipango ya kujiweka tayari kwa ajili ya michuano hiyo, huku akisema Juni 20 ambayo ndio mwisho wa timu yao kufanya usajili watakuwa wameshakamilisha kila kitu na mashabiki wao wasiwe na wasiwasi.

“Tumeshaanza vikao kujadili nini kinatakiwa kufanyika ili tuweze kuendana na mipango ya CAF, lakini naamini kuanzia Juni 15 mwaka huu tutakuwa tunafahamu nini kinatakiwa na nini hakitakiwi, kwani ndiyo mipango rasmi itaanza kufanyika,” alisema bosi huyo aliyefanya kazi kubwa kwenye timu hiyo msimu huu.

Hata hivyo, taarifa hiyo imezitangaza nchi 12 ambazo zinaingiza timu nne kwenye michuano hiyo msimu huu.

 Imezitangaza Algeria, Angola, Ivory Coast , Misri, Libya, Morocco, Nigeria, DR Congo, Afrika Kusini, Sudan, Tunisia na Tanzania.

Related Posts