Iringa. Bodi ya Usajili wa Makandarasi Tanzania (CRB), imewaonya makandarasi kwenye tabia ya kutumika na kampuni za kigeni katika usajili wa ukandarasi, ili kampuni hizo zionekane za kizawa.
Onyo hilo limetolewa leo Jumatano Juni 5,2024 na Msajili wa CRB, Rhoben Nkori wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa makandarasi kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yanayofanyika kwa siku tatu mkoani Iringa.
Amesema wapo baadhi ya wataalamu kwenye kampuni za ukandarasi hudanganya kuwa na wanahisa kati ya asilimia 51, ili kampuni zibadilishwe na kuwa za kizawa wakati wakijua wameahidiwa mishahara pekee.
Nkori amesema kufanya hivyo ni kosa kisheria na kwamba atakayebainika atafutiwa kampuni iliyosajiliwa na kufungiwa, ili asisajili kampuni nyingine ndani ya miaka mitatu.
“Hakuna anayekuzuia kama muungano wenu ni wa kibiashara. Unapewa hisa ubadilishe kampuni iwe ya kizawa unakubali, wakati unajua unachopata ni mshahara peke yake,” amesema na kuongeza;
“Unachofanya ni kuidhulumu nafasi yako, unawadhulumu Watanzania wenzako na unaidhulumu nchi yako, unakuwa mbele ili kampuni iwe ya kizawa wakati sio ya kizawa.”
Aidha, msajili huyo wa CRB amewatoa hofu kuwa kinachozungumzwa na Serikali kuhusu makandarasi wazawa kupewa kipaumbele kwenye kazi ni kweli.
“Kila mmoja amesikia jitihada za Serikali jinsi ya kuwezesha makandarasi wazawa sio siasa, ni kweli na sisi tulio ndani tunaona.
“Cha msingi watakaobahatika kufanya kazi kwa awali wawe waaminifu kuiaminisha Serikali kwamba makandarasi wa ndani tunaweza na hiyo itaongeza imani kwa Serikali na baadae fedha zinazokwenda kwa makandarasi wa nje, zitakuja ndani,” amesisitiza.
Awali, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (CRB), Nisile Mwandetele amesema mafunzo hayo ni muhimu na yanalenga kuimarisha kazi ya ukandarasi.
Amewataka makandarasi hao kuwa waaminifu wanapopewa kazi.
Kwa upande wao, baadhi ya makandarasi wamesema mafunzo hayo ambayo hutolewa mara kwa mara yamekuwa yakiwaimarisha katika utendaji wao, tofauti na kama yasingekuwepo.
“Binafsi mafunzo yamekuwa muhimu sana kwangu na sijawahi kukosa tangu niwe mkandarasi,” amesema Vitus Mushi, mmoja wa makandarasi.