Dodoma. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameziagiza halmashauri nchini kusimamia ipasavyo sheria ndogo za mazingira na kuchukua hatua kwa wale watakaobainika kwenda kinyume na sheria hizo.
Mbali na hilo , amesema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021/22 takribani eneo la kilometa za mraba la 95,793 zilichomwa, huku mikoa Morogoro, Katavi na Lindi ikitajwa kuwa na sehemu kubwa iliyochomwa moto.
Dk Mpango ameyasema hayo leo Juni 5, 2024 wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.
“Halmashauri zisimamie ipasavyo sheria ndogo za kulinda mazingira na kuhakikisha kuwa hatua za kisheria dhidi ya wale wanaokwenda kinyume. Na kila mwananchi awe mlinzi wa mwenzake kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayetupa taka ovyo na kuchafua mazingira yetu,”amesema.
Ameziagiza pia halmashauri nchini kuhamasisha viwanda vyenye teknolojia za kubadili takataka mbalimbali ili ziweze kutumika tena kama bidhaa.
Amewataka pia wananchi na sekta binafsi kuchangamkia fursa za ukusanyaji na urejelezaji wa taka ili kutengeneza bidhaa.
Dk Mpango amesema licha ya hatua mbalimbali zinazofanyika za kuhifadhi mazingira, uharibifu wa mazingira na uoto wa asili kupotea kwa baadhi ya viumbe hai, uchafuzi wa mazingira bado umeendelea kuongezeka kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya mkaa kwa ajili ya kupikia, kilimo, ufugaji wa kuhamahama na uchomaji ovyo wa misitu.
Amesema kiwango cha upotevu wa maeneo ya misitu kimeongezeka kutoka hekta 372,816, mwaka 2019 hadi kufikia 469,420 katika mwaka 2023.
Mbali na hilo amebainisha kuwa kiwango cha matumizi ya kuni na mkaa kimeongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na ongezeko la watu ambapo takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2021/22 takribani eneo la kilometa za mraba la 95,793 zilichomwa.
Amesema sehemu kubwa ya uchomaji wa moto ilifanyika katika mikoa ya Katavi, Lindi na Morogoro kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo uandaaji wa mashamba malisho ya mifugo na uwindaji na urinaji wa asali.
Dk Mpango amesema kwa Tanzania takwimu zinaonyesha kaya tisa, kati ya 10 hutumia mkaa ama kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.
Pia amesema takwimu zinaonyesha kati ya watu 100 ni wanane tu wanaotumia nishati safi.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Tanzania na barani Afrika.
Amesema Rais Samia ameagiza itakapofika mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia.
Amesema ili kuhakikisha hayo yanafanikiwa aliunda kamati ya Taifa itakayosimamia suala hilo na kuanzisha Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia itakayoweka ruzuku kwa wananchi wa kipato cha chini kumudu.
Akizungumzia madhara ya kutupa plastiki baharini, Mpango amesema takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya plastiki baharini itakuwa kubwa kuliko samaki ifikapo 2050.
Amesema suala hilo linahatarisha viumbe hai na binadamu kwa kuwa zinatengeneza sumu ambazo zitawaathiri.
Dk Mpango amesema ili kufanikisha kuhuisha ardhi iliyoharibiwa na kujenga ustahimilivu wa ukame na kuzuia kuenea kwa jangwa, ni muhimu kwa Taifa kuimarisha menejimenti na usimamizi wa mazingira.
Amesema kuimarisha huko kutatokana na kuhakikisha kupima na kuzingatia matumizi bora ya ardhi na kubadili mfumo wa ufugaji kwa kufuga kisasa.
“Ni lazima kubadili kilimo chetu kuwa endelevu na cha kisasa zaidi kinachozingatia mboji na marejea, matumizi ya matandazo ya majani ili kuhifadhi unyevunyevu na matumizi ya teknolojia ya kijani, udhibiti wa uchomaji ovyo wa misitu na vichaka,”amesema.
Amesema pia kutunga sheria ndogo za utunzaji wa mazingira na udhibiti wa taka na kuwataka viongozi wa Serikali, Bunge, sekta binafsi kuungana ili kutoa elimu kwa umma juu ya utunzaji wa mazingira.
Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuweka mazingira safi yanaowazunguka wakati wote na kutumia nishati safi ili kuokoa mazingira.
Aidha, amesema watasimamia na kusisitiza sektarieti za mikoa yote kutekeleza masuala mbalimbali aliyoagiza Dk Mpango katika utunzaji wa mazingira.
Ameyataja mambo hayo ni kuratibu shughuli za usafi wa mazingira katika majiji, wilaya na manispaa na kusimamia sheria za utunzaji wa mazingira.
“Kubuni mbinu zitakazowezesha vijiji miji na majiji kuwa safi ikiwemo na utenganishaji wa taka katika vyanzo vya uzalishaji taka,”amesema.
Amezitaka sektarieti za mikoa pia kutengeneza mazingira wezeshi ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika udhibiti wa kuzagaa kwa taka katika maeneo yao.
Pia amewataka kuandaa mpango mahususi wa ushirikishwaji wa kila kaya wa kushiriki katika usafi wa mazingira.
Mengine ni udhibiti wa taka pamoja na utunzaji na kuendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi ambayo ni gesi umeme na makaa ya mawe.