Moshi. Wimbi la magari ya kifahari kutumika kusafirisha wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, linazidi kushika kasi nchini na safari hii gari linalodaiwa kuwa la Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likikamatwa na wahamiaji haramu saba.
Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilikamatwa jana saa 2:00 asubuhi katika hoteli moja iliyopo Njiapanda ya Himo, Barabara ya Moshi-Dar es Salaam Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, lakini wakati likikamatwa, mbunge huyo hakuwemo ndani ya gari.
Alipotafutwa na Mwananchi, Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga amekiri kuwepo kwa tukio hilo na ameomba apewe muda mpaka leo Jumatano, ndiyo alizungumzie suala hilo kwa kina baada ya kukusanya taarifa kamili.
“Ni kweli kuna tukio kama hilo. Naomba tuonane kesho (leo) nikishaweka mambo vizuri. Siwezi kuzungumza hapa kwa sasa. Kuna mambo hayajakaa sawa ila kweli hilo tukio (la kukamatwa kwa gari la Mbunge) lipo,” amesema Kamanda Nyakunga.
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa hazikuzaa matunda, kila alipopigiwa simu alijibu yuko kwenye msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.
Taarifa kutoka eneo la tukio, zilidokeza kuwa wahamiaji hao haramu kutoka Ethiopia walikamatwa jana asubuhi nje ya hoteli hiyo iliyopo Njiapanda na ndani ya gari walikutwa wahamiaji haramu saba.
Kulingana na taarifa hizo, hoteli hiyo inazo kamera za ulinzi (CCTV), ambapo kulingana na mienendo ya dereva wa gari hilo na taarifa ambazo polisi walikuwa nazo, walilizingira gari hilo na kuwakuta wahamiaji hao.
“Huyu dereva alikuja, akaegesha gari hapo nje akashuka kwenda kununua vocha kwa ajili ya simu yake. Hata hivyo, inaonekana polisi walikuwa wakilifuatilia kwa sababu baada ya kupaki haukupita muda, maofisa hao walijitokeza,” kimedokeza chanzo chetu kutoka eneo la tukio.
Dereva huyo aliporudi kwenye gari, baada ya muda mfupi alitokomea kusikojulikana na uchunguzi wa awali unaonyesha gari hilo linamilikiwa na mbunge (jina lake linahifadhiwa kwa sasa).
“Baada ya kubainika kuwa ni gari ya mbunge (jina tunalo) ndiyo sasa mawasiliano ya wakubwa yakafanyika, kwa hiyo hatujui nini kinaendelea ila ukiwauliza Polisi au Uhamiaji utapata nini kinaendelea,” kilidokeza chanzo hicho.