Dodoma. Serikali imetaja mikakati inayotekeleza kupunguza ajali za barabarani, ikiwamo kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, amesema hayo leo Juni 5, 2024 alipojibu swali la msingi na mbunge wa Viti Maalumu, Felista Njau.
Katika swali la msingi, Felista amehoji Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kukomesha kabisa ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi.
Sagini amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti itakayosaidia kukomesha ajali za barabarani ambayo ni pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani ambayo muswada umeshawasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza.
Amesema mkakati mwingine ni kuboresha miundombinu ya barabara na kuweka alama za matumizi ya barabara, kuandaa utaratibu wa kufunga mifumo ya Tehama barabarani ili kufuatilia na kudhibiti ajali.
“Kuandaa utaratibu wa ukaguzi wa lazima wa vyombo vya moto ili kudhibiti ubora wa vyombo hivyo viwapo barabarani, na kuendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia vituo vya runinga na redio, na elimu kwenye shule za msingi.
Sagini amesema elimu pia inatolewa kwa shule za sekondari na vyuo, vituo vya mabasi, vituo vya bodaboda na bajaji, vituo vya ukaguzi wa magari, shule za udereva na kutoa mafunzo kwa madereva wa Serikali, taasisi za umma na watu binafsi.
Katika swali la nyongeza, Felista amesema ajali nyingi zimekuwa zikitokana na bodaboda ambao hawana muda wa kusikiliza redio, hivyo amehoji mkakati wa Serikali kuwezesha kupata elimu na kuepuka athari.
Pia amesema kumekuwa na ucheleweshaji wa utoaji nyaraka kutoka polisi kwa watu wanaopata ajali wakiwemo bodaboda.
Amehoji mkakati wa Serikali wa kuhakikisha wanapata nyaraka hizo kwa wakati kunusuru afya za watu.
Sagini amesema ipo tabia ya vijana wa bodaboda kuanza kuendesha vyombo hivyo bila kupita chuoni, akieleza ndiyo maana wameandaa mkakati wa kuwapa mafunzo wakiwa katika vituo vyao.
Kuhusu nyaraka za bima kuchelewa, amewaagiza makamanda wa polisi mkoa kuhakikisha makamanda wote wa trafiki wa mikoa na wilaya wasiwe vikwazo vya kuchelewesha nyaraka hizo.
Mbunge wa Ilemela, Dk Angelina Mabula amesema ajali nyingine za barabarani zinatokana na bodaboda kutokuwa na maeneo ya maegesho, hususani katika viwanja vya ndege.
Amehoji iwapo Serikali haioni ni muda sasa wa kutenga maegesho ya bodaboda na bajaji karibu na maegesho ya magari ili kuepuka ajali zinazotokana na kugombea abiria.
Sagini amesema hoja hiyo ni ya msingi na kwamba, wamewahi kuzielekeza halmashauri kutenga maeneo mahususi kwa ajili ya bodaboda.
Amesema kuna maeneo wamestaarabika kwa kutenga maeneo ya bodaboda na bajaji, kwa kuanzisha vikundi vilivyoweka mfumo wa upakiaji abiria.