KIUNGO wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye amepachika mabao 19 msimu huu akisema ndio msimu wake bora licha ya kukosa mataji, ametaja kikosi bora chake cha msimu akiwajumuisha nyota saba wa Yanga, watatu wa Azam na mmoja wa KMC, ambao anaamini wakicheza mechi hakuna wa kuwazuia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei Toto, amesema alikuwa na msimu mzuri kuliko misimu yote aliyocheza Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya kukosa mataji.
“Tangu nimeanza kucheza soka la ushindani sijawahi kufunga idadi kubwa ya mabao kama msimu huu hivyo nakiri kuwa huu ndio ulikuwa bora na wa ushindani kwangu nafurahi nimeumaliza salama,” alisema na kuongeza;
“Nimekutana na wachezaji wengi bora na wamenipa changamoto kutoka timu pinzani ni wengi wamefanya vizuri lakini kuhusu kikosi bora haya ni maoni yangu binafsi,” alisema.
Akitaja kikosi hicho, Fei Toto alisema langoni anaanza na Djigui Diarra kipa namba moja wa Yanga, Attohoula Yao, Pascal Msindo, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Yeison Fuentes, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Fei Toto na Wazir Junior wa KMC.
“Siwezi kumuelezea mchezaji mmoja mmoja kwanini nimemtaja nafikiri namba zao zinajieleza namna walivyozisaidia timu zao na huo ni mtazamo wangu mimi,” alisema Fei toto.
Mwanaspoti linakuletea takwimu za mastaa hao aliowataja Fei Toto kwa namba na timu wanazocheza kwa kuanza kipa hadi mshambuliaji.
Diarra ni moja ya makipa bora kwa sasa katika Ligi Kuu Bara. Ameshinda tuzo ya Glovu za Dhahabu ya Kipa Bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo na msimu huu alikuwa anawania kwa mara ya tatu mfululizo akiwa na ‘clean sheets’ 14, kabla ya kupitwa katika mechi ya mwisho ya kufungia msimu na Ley Matampi wa Coastal Union mwenye ‘clean sheets’ 15.
Yao ambaye huu ni msimu wake kwanza hapa nchini tangu ajiunge na Yanga akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast amekuwa ni moja ya mabeki bora wa kulia ambapo amefunga bao moja la Ligi Kuu Bara huku akitoa asisti za mabao mengine saba. Ndiye beki aliyechangia mabao mengi zaidi msimu huu.
Ni beki ambaye amejitengenezea ufalme wake ndani ya kikosi cha Azam FC hili limethibitishwa baada ya uongozi na benchi la ufundi kuvutiwa na uwezo wake na kuamua kumuongeza mkataba ambao utamuweka ndani ya timu hiyo hadi 2027.
Tangu nyota huyo amesajiliwa na Yanga Januari 14, 2022 akitokea klabu ya KMKM ya Zanzibar hakuna ubishi kwamba amekuwa tegemeo katika eneo la beki wa kati wa timu hiyo. Kiwango chake bora ndicho kilichowafanya mabosi wa Yanga kumuongezea mkataba hadi 2027 wakiamini atakuwa chachu ya mafanikio.
Ni usajili mpya ndani ya kikosi cha Azam FC msimu huu uliohitimika hivi karibuni, amecheza miezi sita kutokana na kuingia ndani ya timu hiyo katika dirisha dogo la usajili na ndani ya miezi hiyo amefanya kazi kubwa akiipambania timu yake kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.
Hii ndio injini ya Yanga msimu huu na amekuwa katika kiwango bora kikosini humo licha ya kupambana na wachezaji nyota wa timu hiyo wakiwemo, Jonas Mkude, Zawadi Mauya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambao wote wamekuwa wakisubiri kwa Mganda huyo.
Licha ya kukosekana kwenye baadhi ya mechi kutokana na kusumbuliwa na majeraha kiungo huyo ametajwa kwenye kikosi cha mastaa 11 bora wa msimu huu, kiungo huyo mshambuliaji ndani ya kikosi cha Yanga amepachika mabao saba na amethibitisha ni kiungo fundi sana mwenye kipaji cha kipekee.
Anaingia pia katika kikosi bora cha Fei Toto kutokana na namba alizochangia kwenye kikosi cha Yanga akipachika mabao 11 ya Ligi Kuu Bara huku akiwa ni miongoni mwa mastaa waliocheza mechi nyingi ndani ya timu hiyo.
FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’ (AZAM FC)
Huu ni msimu bora kwa nyota huyu aliyetua Azam FC msimu uliopita akitokea Yanga ambapo tangu amejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam amehusika katika jumla ya mabao 26, akifunga 19 na kutoa asisti saba, kati ya mabao 63 yaliyofungwa na timu nzima.
Ameshinda tuzo ya Kiatu cha Dhahabu cha Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara akihusika katika jumla ya mabao 29 kati ya 67 yaliyofungwa na timu nzima akiwa amefunga 21 na kutoa asisti nane katika mechi 27 alizocheza msimu huu ikiwa ni msimu bora zaidi kwake ndani ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.
Mastraika hawakuwa na msimu bora sana na walikimbizwa na viungo kwenye upachikaji wa mabao. Lakini huyu hapa ni straika Na.9 pekee aliyetingisha msimu huu akifunga mabao 12 na kuwa ndiye mshambuliaji pekee miongoni mwa waliokuwa katika nafasi tatu za juu za waliowania tuzo ya mfungaji bora akizidiwa na Stephane Aziz Ki wa Yanga (21) na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC mwenye 19.