Majibu ya Bashe kwa Mpina uagizaji sukari nje

Dodoma. Serikali imeweka msisitizo ikisema changamoto iliyojitokeza mwanzoni mwa mwaka huu ya bei ya sukari kupaa halitajirudia.

Kauli hiyo imetolewa baada ya hoja kuhusu sukari kujitokeza wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2024/25 bungeni jana Juni 4, 2024.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina amesema kuruhusiwa wafanyabiashara kuagiza sukari kutaua viwanda nchini.

Waziri wa Kilimo, Hussen Bashe aliainisha mipango ya Serikali kuzuia upandaji wa bei ya sukari kama ilivyotokea Desemba, 2023 hadi Februari, 2024, kuwa  ni kuagiza tani 410,000 za bidhaa hiyo hadi kufikia Desemba mwaka huu.

Amesema Serikali italinda walaji, wakulima, viwanda na wafanyabiashara.

Bashe amesema mfumo wa usambazaji na uzalishaji wa sukari wataulinda kuondoa mfumo hodhi ambao kila mkoa utakuwa na msambazaji.

Amesema kila kiwanda kitakuwa hakijiamulii bei kinavyotaka kwa kuwa Serikali italisimamia jambo hilo.

Akieleza kilichosababisha uagizaji sukari kufanyika, Bashe amesema awali walikisia kuwa upungufu wa sukari utakuwa tani 140,000.

Amesema baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa utabiri wa hali ya mvua, uzalishaji ulianza kushindikana kuanzia Oktoba 2023 hadi Machi mwaka huu.

Hata hivyo, hali ya kukosa uzalishaji imeendelea kwa miezi minane.

Bashe amesema kwa siku wastani wa matumizi ya sukari ni tani 1,500, hivyo kwa mwezi ni tani 45,000 ambayo ukizidisha kwa miezi minane inakuwa zaidi ya tani 350,000.

“Mwaka 2022/23 kulikuwa na upungufu wa tani 60,000 za sukari wakati bei ya rejareja ilikuwa Sh2,600 na viwanda vilipoacha kuagiza, bei ya sukari ilipanda hadi Sh3,000 kwa rejareja,” amesema.

Amesema walipowapa tena vibali vya kuagiza sukari hawakuagiza, hivyo kuanzia Januari na Februari bei  ilipanda na kufikia Sh10,000.

Bashe amesema viwanda vilivyopewa vibali vya kuagiza sukari vilionekana kula njama ya kupanga bei kwa baadaye kuingiza sukari lakini wakaifungia kwenye maghala.

“Tumeenda na polisi kufungua maghala yao walikoficha sukari. Siwezi kuwa waziri ‘boya’ kuangalia wananchi wanavyoumizwa,” amesema.

Bashe amesema viwanda kwa ajili ya kula njama ya kupanga bei, vimeweka msambazaji mmoja wa sukari kwa mikoa zaidi ya 10.

Amesema Serikali ilibadilisha kanuni na kuwapa kazi ya kuagiza sukari Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuagiza tani 410,000 za sukari.

“Tunaenda kuweka utaratibu wa kuondoa njama za kupanga bei kwa kila mkoa kuwa na msambazaji wa sukari,” amesema.

Awali, akichangia Mpina amesema wasipolinda viwanda vya ndani hawawezi kukusanya kodi na kuwa Serikali imeruhusu uagizaji wa tani 410,000 za sukari katika mwaka huu.

Amesema wakati Serikali inafanya hivyo katika mwaka wa fedha 2023/24 Tanzania inahitaji tani 120,000 tu za sukari.

Mpina amesema sheria inataka uagizaji wa sukari kutoka nje kuwa ni wa kiasi kinachopungua tu na kwamba, zaidi ya hapo ni kuamua kuua viwanda vyote vya sukari.

“Maana yake umeamua wakulima wa nchi hii wakose soko, maana yake umeamua wafanyabiashara wafunge viwanda vyote saba bado wadaiwe mikopo mikubwa waliyokopa kwa sababu hawawezi tena kuhimili katika ushindani wa namna hiyo,” amesema.

Amesema kwa taarifa zilizopo wafanyabishara wanaozalisha sukari nchini wanalipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), huku wanaoagiza wakiwa wameondolewa.

“Mbaya zaidi kwa marekebisho ya Sheria ya Sukari ya mwaka 2020 tulishaamua waagizaji wa sukari wawe wenye viwanda tu, lakini hadi sasa wametoa kibali cha wafanyabiashara kuagiza sukari nje ya nchi tofauti na sheria zetu,” amesema.

Mpina amehoji wafanyabiashara hao wameruhusiwa na nani kufanya hivyo.

Related Posts