Mufindi. Katika kuadhimisha kilele cha siku ya Mazingira Duniani, Halmashauri ya Mji Mafinga Wilayani Mufindi, Iringa, imeng’oa miti iliyopandwa kimakosa katika chanzo cha maji cha Iyasambwe.
Imeelezwa kuwa miti hiyo si rafiki kwa vyanzo vya maji kwa sababu inaweza kuvikausha vyanzo hivyo.
Akizungumza baada ya kumaliza kazi hiyo leo Jumatano Juni 5, 2024 katika chanzo cha maji cha Iyasambwa katika kitongoji cha Makwawa, Mkuu wa kitengo cha usafi na udhibiti wa taka ngumu wa Halmashauri hiyo, Charles Tui. amesema wameamua kuondoa miti hiyo ili isiendelee kuharibu chanzo hicho.
“Miti hii tuliyoiondoa leo ni aina ya milingoti iliyopandwa kimakosa pamoja na mianzi, lakini pia kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, inataka kusiwe na shughuli yoyote ya kibinadamu karibu na chanzo cha maji, inatakiwa iwe nje ya mita 60,” amesema Tui.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Rungemba, Justine Ugusi amesema wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika chanzo hicho cha maji na mwaka huu wamepanda miti aina ya mivinge zaidi ya 600 kwenye chanzo hicho.
“Leo tumeadhimisha siku hii ya mazingira kwa kukata miti ambayo sio rafiki ikiwemo mianzi ambayo baada ya kuing’oa tutateketeza mazalia ya mianzi kwa kuimwagia chumvi isiote tena,” amesema Ugusi.
Amewataka wananchi wa kijiji hicho kuendelea kutunza na kulinda chanzo hicho pekee cha maji katika kijiji hicho sambamba na kupanda miti rafiki na maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye Mkazi wa kijiji hicho, Roza Lumati amesema upandaji wa miti una manufaa makubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Amesema mpaka sasa wakazi zaidi ya 2,000 wamenufaika na huduma ya maji yanayotoka kwenye chanzo cha Iyasambwe.