UONGOZI wa Pamba umeanza kufanyia tathimini ya kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara huku ikiwa katika mazungumzo na aliyekuwa Kocha wa Tabora United Mserbia, Goran Kopunovic kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mbwana Makata.
Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zililiambia Mwanaspoti, viongozi wameanza kukaa vikao kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali huku mazungumzo na Goran yakifanyika kwa siri baada ya kutokuwa na imani na Mbwana Makata aliyewapandisha.
“Ni kweli tumekuwa na mawasiliano na Goran kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mbwana Makata ambaye mkataba wake umeshafikia ukomo, majadiliano bado yanaendelea na tutakapofikia muafaka juu ya hilo basi tutaliweka wazi,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Pamba, Bhiku Kotecha alisema, kwa sasa kinachoendelea ni vikao vya ndani kwa ndani katika timu hiyo na kila kitu kitakapokamilika wataweka wazi ila mashabiki wa kikosi hicho watarajie mambo mazuri.
“Ni mapema sana na siwezi kusema tutafanya nini lakini tuna malengo ambayo sisi kama viongozi tumeyaweka na tunayafanyia kazi baada tu ya msimu huu kuisha, mashabiki na wadau wetu waendelee kutusapoti kwani mambo mazuri yanakuja,” alisema.
Makata aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya kusota kwa miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, mkataba wake umeisha jambo ambalo viongozi wameanza mazungumzo mapema na Goran kwa ajili ya msimu ujao.
Goran aliyewahi kuifundisha Simba mwaka 2015, aliachana na Tabora United Machi 21, mwaka huu huku akiiongoza timu hiyo katika michezo 21 ya Ligi Kuu Bara ambapo alishinda minne, sare tisa na kupoteza minane akiiacha nafasi ya 13 na pointi 21.
Pamba imepanda Ligi Kuu Bara baada ya kushika nafasi ya pili na pointi 67 nyuma ya vinara KenGold iliyojikusanyia pointi 70.