Simba, Yanga zaletewa bure mastaa 22 wa Safari Cup Dar

BAADA ya mchujo mkali kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania hatimaye kikosi cha mastaa wapya vijana 22 wa mashindano hayo ya kuibua vipaji vya soka maarufu kama Kombe la Safari Lager Tanzania wametajwa.

Mastaa hayo tayari wameingia kambini jijini Dar es Salaam na watakuwa chini ya malijendi kadhaa wa Tanzania akiwemo winga wa zamani wa Taifa Stars, Mrisho Ngassa na klabu mbalimbali ikiwamo Simba na Yanga zinaruhusiwa kuwanyakua kwa idadi wanayotaka.

Tangu Oktoba 2023, kombe hilo lilichezwa katika mikoa mbalimbali ikisimamiwa na makocha maarufu wa Tanzania ambao walipata idadi kubwa ya wachezaji wapya wa soka na kuwachuja mpaka kufikia idadi hiyo kwa kutumia vigezo maalum ambapo baada ya mechi za kirafiki jijini Dar es Salaam klabu mbalimbali zitaruhusiwa kusajili wachezaji hao kwa makubaliano maalumu.

Baadhi ya kanda zilizofanyiwa mchujo huo katika maeneo maalum ni Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam ambapo idadi hiyo imetoka kwenye wachezaji 64.

Kwa mujibu wa waandaaji, miongoni mwa vigezo vilivyotumiwa na makocha ni pamoja na ujuzi wa mchezaji husika, uwezo wao wa kuvumilia katika hali tofauti, umri pamoja na kujitolea kwao katika michezo ya ushindani.

Baada ya mchujo mkali na uchunguzi wa wachezaji, wachezaji hao wataingia kwenye kambi ya mafunzo ya wiki tatu ambapo watapewa mafunzo na wataalamu wa lishe, washauri wa kifedha na wachezaji maarufu wa zamani.

Kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Safari Lager, mashabiki wataweza kuona safari ya timu hiyo ya mabingwa ya Safari Lager, kujifunza kuhusu wachezaji, kuona picha na video za nyuma ya pazia.

Meneja wa Safari Lager, Abigail Mutaboyerwa, alisema; “Safari Lager Cup ni zaidi ya mashindano ya soka, tunajivunia kuwasilisha timu ya mabingwa ya Safari Lager na kuwaalika taifa kuwaunga mkono.”

Kikosi; Abubakary Lyanga (Dar es Salaam), Edmund Zephania (Arusha), Steven Claudia  (Mwanza), Benson Burton(Dar es Salaam), David Shiraji (Arusha), Mathias Anthony (Dar es Salaam), Kisumo Anthony(Mwanza), Jeremiah James (Mbeya), Baraka Thobias (Mbeya), Augostino Anderson (Arusha) na Somji Hailonje (Mbeya).

Wengine ni Samson Kamese (Mbeya), Festo Mkumbo (Mbeya), Salim Shida Ally (Mbeya), Jacob Mussa Ndege (Mbeya), Hussein Ally (Dar es Salaam), Kelvin Komba (Mbeya), Habib Kingo(Dar es Salaam), Ibrahim Samweli (Arusha), Erick Ponsian (Arusha), Marwa Mwita (Mwanza) na Prince Paul (Arusha).

Related Posts